MIAKA 18 TANGU ASTAAFU UPISHI HAJALIPWA MAFAO YAKE,AMUOMBA RAIS SAMIA AMSAIDIE

 


Mzee Julius Marwa

******


Na Dinna Maningo, Butiama 

MKAZI wa kijiji cha Kiabakari kata Kukirango wilaya ya Butiama mkoa wa Mara ,Julius Marwa  mwenye umri wa miaka (76) amemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu  Hassan kumsaidia ili alipwe mafao yake ya zaidi ya Milioni 35 aliyoyakosa kwa miaka 18 tangu alipostafu kazi ya upishi 2006.

Akizungumza na Malunde 1 blog,Marwa amesema kuwa alianza kazi yake ya Utumishi wa upishi katika shule ya msingi Kiagata wilaya ya Butiama na kisha kuhamishiwa katika shule ya ufundi Musoma na kustaafu mwaka 2006.

Marwa amesema kuwa baada ya kustaafu amekuwa akufuatilia mafao yake lakini hajafanikiwa,anamuomba Rais Samia amsaidie ili apate fedha zake akiwa bado hai na kwamba kwa sasa ameshindwa kuzunguka huku na kule kufuatilia madai yake kwakuwa ni mzee hajiwezi na hana pesa za nauli ili kufuatilia mafao yake.

Amesema kuwa wakati akifuatilia malipo yake uongozi wa shule ya sekondari  Kiagata ulisema kuwa hawezi kulipwa kwa kuwa fedha zake zililetwa shuleni kimakosa hivyo lazima fedha hizo zirudishwe ndipo apewe mafao yake na kwamba baada ya kustaafu mwaka huo hakuwahi kupokea malipo yoyote .

"Nilipofuatilia wengine wakasema kuwa mimi sijaajiriwa ni kibarua,kama nilikuwa kibarua mbona nilipandishwa daraja!? Mhe. Rais Samia mimi ni mzee sijiwezi sina nguvu za kutembea kuzunguka huku na kule kufuatilia mafao yangu,msaada wangu ni wewe,naomba unisaidie nipate pesa ningali hai mimi ni mzee wakati wowote ninaweza kufa,niko hai lakini sijalipwa pesa zangu je nikifa nitalipwa?" Alihoji Marwa.

Mzee huyo amesema kuwa alishafika Ofisi zote alizotakiwa kufika lakini alichoambulia ni kufunguliwa akaunti za benki na kupewa kadi za ATM kwa madai kuwa atawekewa fedha zake lakini hadi sasa hakuna kiasi chochote cha fedha kilichowekwa kwenye akaunti.

"Nimefuatilia sana tangu 2007 bila mafanikio nilishafika Wizarani,Hazina Dar es salaam, na makao makuu Dodoma,wakaniambia watashughulikia nirudi nyumbani, mmoja wa hapo hazina pale Dodoma wakanichukua tukaingia kwenye gari yao hadi Benki wakanifungulia akaunti wadhamini walikuwa wao wakasema nirudi kuwa pesa zitawekwa lakini hadi leo hii hakuna pesa.

" Nilipofuatilia mkoani pale Musoma nako wakaniambia mzee pesa zako ziko tayari wewe fungua akaunti,nikafungua tena nyingine nikaenda shule ya ufundi Musoma nikamuomba mwalimu mkuu anisaidie kunielekeza ili nifungue akaunti.

"Kwa sababu wakati mimi nafanya kazi tulikuwa tunalipwa kwa mkono siyo benki,akanisaidia nikafungua wakaniambia mzee pesa zitaingia muda siyo mrefu we rudi nyumbani,kila nilipoenda benki kuangalia sikukuta pesa yoyote",amesema Marwa.

Mzee Marwa amesema kuwa hakukata tamaa mwaka 2020 alienda tena ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mara kukumbushia madai yake ambapo aliombwa asubiri ili lishughulikiwe na akaonyesha nyaraka mbalimbali kama uthibitisho wa malalamiko yake ya madai,ajira yake ya utumushi wa serikali,nyaraka za malipo na kadi za Benk.

Marwa alionesha kadi mbili za benk ya NMB ambazo moja alidai kufunguliwa na watu wa hazina -Dodoma na kupewa kadi ya ATM yenye namba 51710033002 na nyingine aliyofungua Musoma ya 30310036417 zote zikiwa na jina lake la Julius Jacob Marwa.

Nyaraka nyingine ni barua iliyotumwa kwenda shule ya sekondari Kiagata ya tarehe 3/8/2007 kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi yenye kumb.Na.ED/PFSYCA/178/202/01 ikieleza kuhusu madai yake ya mafao.

Barua hiyo imeeleza" Tumeshindwa kushughulikia malipo ya mafao ya mtajwa Julius J.Marwa C/N.7736290 kwa kuwa hujarudisha mishahara yake iliyokuwa ikiletwa kimakosa hapo kituoni kwako.

"Tafadhali rudisha haraka mishahara yote iliyotolewa baada ya yeye kustaafu barua iliyosainiwa na Fidelia  Lukuna kwa niaba ya Katibu Mkuu", imeeleza Barua hiyo.

Barua nyingine ni ya yeye kupandisha daraja iliyoandikwa kutoka Wizara ya Elimu na Utamaduni ya tarehe 8/11/1995 yenye Kumb.Na.ED/PD.12842/8 kwenda kwa Julius Jacob kupitia kwa mkuu wa shule ya sekondari Kiagata S.L.P 420 Musoma yakupandishwa cheo.

Barua hiyo imeleza"Nina furaha kukujulisha kuwa kibari cha kamati maalumu ya Utumishi serikali ya Wizara hii kimetolewa ili upandishwe cheo kuwa Mpishi daraja la ll kuanzia tarehe.1.7.1994 kwa masharti yafuatayo;

(1) Cheo hiki kina ngazi ya mshahara wa 05.2 yaani Shs.10815 hadi Shs.11,655 kwa mwezi.

"Mshahara wako utarekebishwa kwa mujibu wa kanuni E.16 na waraka wa Watumushi wa serikali Na.3 wa 1992.

(Il) Kanuni na masharti yako mengine yatabadilika,barua iliyosainiwa na M.Mtavangu kwa niaba ya Katibu mkuu."imeeleza barua hiyo.

Januari,30,2018 Mzee huyo aliandika barua kwenda kwa katibu mkuu Wizara ya Elimu yenye Kumb.Na.JLS/MSM/22 ikikumbushia mafao yake ikisema" mimi nilikuwa mtumishi kama Mpishi katika shule ya sekondari kiagata,nikastaafu nikiwa shule ya sekondari Musoma tarehe 10,03,2006.

"Nimejitahidi kila njia kufuatilia madai yafuatayo lakini bado sijafanikiwa kuyapata ambayo ni malipo ya kustaafu kiinua mgongo Tshs.6,769,000,Uhamisho kutoka Kiagata-Musoma 1,903,000, Nauli baada ya kustaafu Musoma-Kiabakari 500,000,Posho ya kujikimu 25,650,000,jumla ya fedha zote ni Milioni 34,822,000 hesabu zilizotayalishwa na chama cha watumishi wa serikali kuu TUGHE " imeeleza barua hiyo.

Kwa mujibu wa barua ya tarehe 21,8,2020 iliyoandikwa na ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Manispaa ya Musoma yenye Kumb.Na.HMM/SE/R.1VOL .1/6/ kwenda kwa Marwa kupitia kwa  Alfred Marwa ikimjulisha kuwa baada ya kupokea barua yake ya  tarehe 30,01,2020,ofisi hiyo imefanya mapitio ya barua hiyo pamoja na nyaraka alizoambatanisha .

Barua hiyo imeeleza kuwa baada ya kuzipitia nyaraka na barua imegundulika Julius Jacob Marwa alikuwa ni Mwajiriwa wa Katibu Mkuu,Wizara ya Elimu na Ufundi ,alikuwa mpishi shule ya sekondari Kiagata,hadi anastaafu utumishi wa umma tarehe 10/03/2006 alikuwa shule ya ufundi Musoma.

Barua imeeleza kuwa kutokana na Maelezo hayo anasisitizwa kufanya mawasiliano na Katibu Mkuu,Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kuhusu madai yake ambaye ndiye anastahili kulipa stahiki zake na siyo mkurugenzi wa halmashauri ya Manispa ya Musoma huku akimtakia ufuatiliaji wenye mafanikio.

Desemba,16,2021ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mara iliandika barua kwenda ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Butiama Kumb.Na.FA 13/48/01/"0"/12 ikieleza malalamiko ya Marwa kutolipwa mafao yake baada ya kustaafu 2006 japo amekuwa akifuatilia suala hilo kwa muda mrefu.

Barua imeeleza kuwa katika nyaraka alizowasilisha ni pamoja na barua Kumb.Na.ED/PF.SYCA/178/202/01 ya tarehe 31,Agosti,2021 kutoka kwa katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya ufundi kwenda kwa mkuu wa shule ya sekondari ya Kiagata iliyoeleza kushindwa kushughulikia malipo ya mafao ya mstaafu kwakuwa mkuu wa shule ya sekondari Kiagata hajarudisha mishahara iliyotumwa kimakosa.

Barua hiyo ilimwelekeza mkurugenzi wa Halmashauri kumtaka mkuu wa shule ya sekondari Kiagata kurejesha fedha kwa katibu mkuu Wizara hiyo ya elimu ili mstaafu huyo aweze kulipwa mafao yake.

"Natarajia kupata taarifa ya utekelezaji wa maelekezo haya kabla ya 30,12,2021,barua iliyosainiwa na Albert G. Msovela Katibu Tawala mkoa wa Mara,Nakala ikielekezwa kwa mkuu wa wilaya ya Butiama kwa ufuatiliaji na kuhakikisha maelekezo hayo yanatekelezwa na kisha ampatie taarifa" imeeleza barua hiyo.

Hata hivyo Marwa amesema kuwa pamoja na jitihada hizo za kufuatilia na barua kadhaa kuandikwa hadi sasa hajapokea malipo yake zaidi tu ya ukimya,anamuomba Rais Samia amsaidie ili alipwe mafao yake.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم