Mama mmoja mkazi wa kata ya Daraja Mbili mkoa wa Arusha anayefahamika kwa jina la Fatma, anadai kuwa ameibiwa mtoto wake na sasa ni zaidi ya miezi sita imepita tangu kumpoteza.
Akizungumza na Millardayo.com Mama huyo ameelezea tukio la kuibiwa mtoto na dada aliyekutana naye njiani.
“Nilikutana na huyo dada, nilikua naenda NMC saa kumi, nilikuwa nimembeba mtoto mgongoni mikono imetoka nje, Yule dada akaniita akaniuliza huyo mtoto ulivyombeba haumii mkono? Nikamwambia haumii, ndiyo akanisogelea badala ya kuenda NMC nikawa namfuata yeye, ” alisema mama huyo.
Amesema, kuna sehemu walipofika akamnunulia pombe na kumwambia yeye anakaa Sakina na kwamba yeye ana mtoto wa kiume ila hana wa kike.
“Nimekaa nae pale, ilivyofika mida ya saa moja na nusu kuelekea saa mbili tukawa tumetoka yeye akiwa amembeba mtoto, ikatokea toyo akasimamisha, akawa amenirudishia mtoto ile nambeba mtoto mgongoni nachukua nguo, akampora mtoto mgongoni akakimbia nae na toyo,” alifafanua mama huyo.
Naye baba wa mtoto huyo, Ramson Mkonyi amesema kuwa wamefuatilia suala la kupotea mtoto Kituo cha polisi wamemdharau.
“Wananidharau sababu mtuhumiwa wangu nimempata, lakini wananitukana, mtuhumiwa ananitukana mbele ya chumba cha mpelelezi,” alisema baba huyo.
Amesema wanaiomba Serikali iwasaidie waweze kumpata mtoto wao kwani kila wanapopeleka mtuhumiwa kituo cha polisi, anaachiliwa bila wao kushirikishwa.
“Mtuhumiwa wa kwanza aliachiliwa bila maelezo yetu sisi, unakutana nae mtaani anacheka na kusema hatumuwezi, wa pili pia ameachiliwa bila kutushirikisha.” Alisema baba wa mtoto.