TANZANIA YAADHIMISHA SIKU YA SARATANI...IDADI YA WAGONJWA YAONGEZEKA

Na Dotto Kwilasa Malunde 1 Blog, DODOMA.

IKIWA ni siku ya  Saratani Duniani,Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa wapya wa Saratani 42,060 kwa mwaka huku takribani wagonjwa 28,610 sawa na asilimia 68 wakipoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.  

Hayo yameelezwa leo Jijini Dodoma na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu wakati akiongea na wananchi kuhusu  maadhimisho ya siku ya Saratani katika kituo cha afya Makole yaliyolenga  kutoa elimu ya kinga na kuelimisha wananchi na hatua za kuchukua kukabiliana na ugonjwa huo. 

Amesema  takwimu kutoka kwenye kanzi data  zilizoanzishwa kwa Kanda , zinaonesha kwamba wagonjwa wapya 14,136 walifikiwa na huduma  ambayo ni sawa na asilimia 33 ya makadirio ya wagonjwa wapya wote kwa mwaka 2021 ikiwa ni ongezeko la asilimia tano ukilinganisha na takwimu za Mwaka 2020 ambapo jumla ya wagonjwa wapya 12,096 (28%) walionwa. 

Waziri huyo pia ameeleza kuwa taarifa za mwaka 2021 kutoka kanzi data ya wagonjwa iliyopo Taasisi ya Saratani ya Ocean Road inaonesha kuwa Saratani zinazoathiri wanaume zaidi ni pamoja na saratani ya tezi dume  (21%), Saratani ya Koo (11.8%),Saratani ya utumbo mkubwa na mdogo (9%) na Saratani ya mdomo na kinywa (7.3%).

Ametaja pia aina ya Saratani inayoongoza  kuwaathiri wanawake ni Saratani ya Mlango ya Kizazi (43%), Saratani ya Matiti (14.2%) na Saratani ya koo (3.8) na kuongezà kuwa ongezeko la wagonjwa wa saratani pamoja na magonjwa mengine yasiyoambukiza, linachangiwa zaidi na mtindo wa maisha usiozingatia afya bora.

"Kuna mtindo mbaya wa maisha unaochangia saratani kama kutokufanya mazoezi (Tabia Bwete), unene uliokithiri, matumizi ya tumbaku na bidhaa zake, matumizi ya pombe kupita kiasi na ulaji usiofaa kama kutokula mbogamboga na matunda, matumizi ya chumvi na sukari kwa wingi,"amesema.

Ameeleza kúwa katika kipindi cha  miaka 10 iliyopita, Tanzania imeshuhudia ongezeko kubwa la wagonjwa wa saratani zinazochangiwa na mtindo wa maisha ikilinganishwa na ilivyokuwa awali ambapo wagonjwa wengi walikuwa ni wale wenye saratani zinazotokana na maambukizi ya virusi,

"Kwa kutambua hilo, Serikali imeongeza juhudi za kuhakikisha kuwa uelewa katika jamii kuhusiana na tatizo hili unaongezeka kwa kuandaa mtaala wa mafunzo mashuleni unaozungumzia magonjwa yasiyoambukiza na namna ya kudhibiti na kuanzisha Program ya taifa ya kuzuia na kudhibiti magonjwa Yasiyoambukiza  yasiyoambukiza ikiwemo saratani,"amesema.

Akieleza takwimu za Dunia,Waziri Ummy amesema takwimu za Shirika la Kimataifa la Utafiti wa Saratani (International Atomic Research on Cancer-IARC) na Shirika la Afya Duniani (WHO), 2018 zinaeleza kwamba kila mwaka duniani kote kunatokea wagonjwa wapya wanaokadiriwa kufikia milioni 18.1, na kati ya hao, zaidi ya wagonjwa milioni 9.6 hufariki kutokana na ugonjwa wa saratani sawa na asilimia 50. 

Katika hilo amesisitiza kila mmoja kupima afya yake mara kwa mara ili kutambua hali yake ya kiafya na kwamba endapo atatambuliwa kuwa una ugonjwa wa Saratani wataoaswa kutumia huduma za afya kulingana na ushauri watakaopewa na wataalam wa afya. 

"Kwa wale ambao  wameshajitambua kuwa na matatizo ya Saratani lakini hawatumii huduma za afya ipasavyo, nawaasa watumie huduma za afya zilizopo kwa manufaa ya afya zao na kuepusha athari zinazotokana na ugonjwa wa Saratani ,na kwa wale ambao hawajapata ugonjwa huu waendelee kuchukua tahadhari kwa kuzingatia kanuni za Mtindo bora wa maisha,"amesisitiza.

Sambamba na hayo Waziri Ummy ameweka msisitizo   kwa watanzania kuchukua hatua za kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza hususan saratani kwa kufanya Kuzingatia ulaji unaofaa kwa kula mlo kamili, ulaji wa matunda na mboga mboga za kutosha, kuepuka ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, kuepuka kula vyakula vyenye chumvi nyingi, na kuepuka ulaji wa vyakula na vinjywaji vyenye sukari nyingi.

Siku ya Saratani Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 4 Februari ambapo ilianza kuadhimishwa mwaka 2000 mjini Paris, Ufaransa wakati wa mkutano wa Dunia wa saratani ,Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Saratani Duniani kwa mwaka 2022 ni Huduma za saratani  sawa kwa wote.’ 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم