VIGOGO WAPISHANA KUCHUKUA FOMU YA UNAIBU SPIKA WHITE HOUSE DODOMA,WAMO KIGWANGALLA,ZUNGU,MWIMYI NA XADAY
Saturday, February 05, 2022
Mbunge wa Nzega vijijini Dkt. Hamisi Kigwangalla akionesha fomu ya kuwania nafasi ya Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ofisi za makao makuu ya CCM jijini Dodoma Mbunge wa Hanang' Mhandisi Samwel Samwel Hhayuma Xaday akiongea na Waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya Naibu Spika.
***** Na Dotto Kwilasa, Malunde 1 Blog-DODOMA. MCHAKATO wa kumpata mgombea wa kiti cha Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM umezidi kupamba moto ambapo wabunge wengi wamejitokeza kuchukua fomu kuomba ridhaa ya kugombea nafasi hiyo.
Baadhi ya Wabunge hao ni Mbunge wa Mahonda Kaskazini Zanzibar Abdallah Ally Mwinyi ambaye amesema amefikia uamuzi huo kwa kuwa ameona ana uzoefu wa kuongoza na hivyo kuamua kuchukua fomu.
Akizungumza leo February 5, 2022 jijini Dodoma mara baada ya kuchukua fomu katika Makao makuu ya chama hicho(White house) Mwinyi amejinadi kuwa ana uzoefu wa miaka 10 bungeni.
"Nina furaha ya kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa na chama changu nafasi ya Uspika,"amesema mbunge huyo.
Amesema anajiamini kwa kuwa ana uzoefu kwenye masuala ya uongozi na kwamba alishawahi kuwa mbunge wa Afrika Mashariki ambalo ni sawa na Bunge la Tanzania na kueleza kuwa utofauti wa mabunge hayo ni lugha tu lile linatunia kiingereza na hili la Tanzania linatumia lugha ya Kiswahili.
Sifa nyingine za Mwinyi ni mwanasiasa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Tanzania, Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama Kuu ya Zanzibar, ambapo aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Haki .
Mwinyi huyo huyo anatajwa pia kuwa mstari wa mbele katika kutetea maslahi ya taifa kwa michango wake wa kutetea kasi ya kujiunga na soko la pamoja ambapo nchi za jirani haswa Kenya na Rwanda walikua wanatukaba shingo kufungua mipaka yetu kwa bidhaa zao, hadi kutetea ongezeko la vibali vya kazi kwa wafanyakazi wageni nchini na kusema kua vibali hivyo ni kwa wafanyakazi wote wakiwemo wa nchi wanachama wa EAC.
Naye Dkt. Hamisi Kigwangwalla ambaye ni Mbunge wa Nzega amesema amejitokeza kuchukua fomu kutokana na kujiona ana uwezo na sifa za kugombea nafasi hiyo na kwamba Chama ndio chenye maamuzi.
Akizungumza na Waandishi wa habari Kigwangalla amejinadi kuwa na uzoefu wa kutosha kwenye Chama na Serikali kwa kuwa Mbunge kwa kipindi cha tatu.
Kwa upande wa Mbunge wa Hanang' Mhandisi Samwel Hhayuma Xaday ameeleza kuwa ana nia ya dhati na watanzania hivyo kuamua kuwa kuchukua fomu ya kuwania kiti hicho cha Naibu Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu hiyo Mhandisi Xaday amesema amechukua uamauzi huo kwa kuwa nafasi hiyo ipo wazi na sifa ya kuwania kiti hicho anayo.
"Nafasi hii ipo wazi baada ya aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge hilo kujiuzulu na kuchaguliwa na chama kuwa Spika nmeona nina sifa ya kuwania nafasi hii Kwa kuwa nnao uzoefu wa kutosha," amesema.
Mhandisi Xaday ameongeza kuwa ikiwa atapata ridhaa ya kuongoza kiti hicho ataisimamia Serikali kupitia ilani ya Chama Cha Mapundizi kwa kuwa yeye ni daraja kati ya wananchi na Serikali.
Mbunge huyo wa Jimbo la Hanang' amekuwa mdau wa michezo kwa kuwahamasisha vijana kuthamini michezo na kuifanya kuwa ajira ya kudumu ambayo inaweza kubadilisha maisha na kuwapatia vipato vikubwa.
Aidha,katika kipindi chote jimboni humo amekuwa akijikita kutangaza utalii na kukuza uchumi wa wilaya ya Hanang na mkoa wa Manyara kwa ujumla kupitia sanaa, michezo na utamaduni.
Pamoja na orodha hiyo yumo pia Mbunge wa Jimbo la Ilala Mussa Zungu , na David Kiyenzele wa Jimbo la Mufindi Kusini ambao Kwa pamoja wameeleza kuwa na nia ya kupata nafasi hiyo kwa kuwa uwezo wanao na nia pia wanayo.
Hatua hii imetokana na Katibu wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa,Itikadi na uenezi Shaka Hamdu Shaka jana(Feb 4,2022)kutangaza ratiba ya mchakato wa kumpata mgombea wa nafasi hiyo kupitia chama hicho.
Kulingana na Shaka ameeleza kuwa wagombea wanatakiwa kuchua fomu na kuzirejesha kuanzia Feb 4-6,2022 kuanzia asubuhi hadi saa tisa alasiri huku Feb 7,2022 ikiwa ni siku ambayo Sekretarieti ya Halmashauri kuu ya CCM itakaa kujadili wagombea na kuishauri kamati kuu ya CCM taifa.
Katibu huyo wa uenezi ameeleza kuwa Feb 8,2022 kutakuwa na tukio la Kamati kuu ya Halmashauri kuu ya CCM Taifa kuchuja na kufanya uteuzi wa mwisho wa wagombea ambapo Feb 10,2022 Kamati ya wabunge wa chama hicho itapiga kura kupitisha jina la Naibu Spika.
Hatua ya uchukuaji fomu ya kugombea nafasi ya Naibu Spika imekuja kutokana na Januari31 Mwaka huu aliyekuwa Naibu Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson kujiuzulu nafasi hiyo kwa mujibu wa Ibara ya 149kifungu Cha kwanza C na Cha pili Cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kuteuliwa kuwa MGOMBEA wa nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Social Plugin