.Na John Walter-Babati
Mashindano maarufu ya kusaka warembo yanayodhaminiwa na kinywaji cha Sed Pineapple flavour Gin kinachozalishwa na kampuni ya Mati super Brand Ltd,kwa mwaka 2022 yamempata mrembo mpya Jenipher Mmari kutoka mkoa wa Kilimanjaro akimvua Annet Japheth wa Manyara aliyekuwa na taji hilo mwaka 2021.
Mrembo huyo amenyakua taji la Mashindano hayo (Sed Miss Valentine’s 2022) yaliyofanyika usiku wa wapendanao (Valentine day) katika ukumbi wa River Nile Hall mjini Babati ambapo amewashinda Warembo wenzake 14 waliokuwa kwenye kinyang’anyiro hicho ambacho kwa msimu huu yalihusisha nchi nzima.
Mara baada ya ushindi, Jennifer Mmari alipatiwa zawadi ya shilingi Milioni moja taslimu huku mshindi wa pili akipata shilingi laki Tano, wa tatu Laki tatu na washiriki wengine wakipatiwa kifuta jasho cha shilingi laki moja kila mmoja.
Mrembo huyo ambaye alibubujikwa na machozi ya furaha wakati anatangazwa kuwa mshindi amesema hakutarajia kupata ushindi kwa kuwa walioshiriki wote walikuwa na uwezo.
Kampuni ya Mati super Brand Ltd huwapatia ubalozi washindi watatu wa mashindano hayo ambayo huandaliwa kila mwaka na kampuni ya Shaba Entertainment chini ya mkurugenzi Shabani Masongo.
Mgeni rasmi katika mashindano hayo ambaye ni Katibu tawala wa Wilaya ya Babati Khalfani Matipula aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Manyara Makongoro Nyerere ameipongeza kampuni ya Mati Super Brands Limited kwa kudhamini mashindano hayo.
Matipula amewataka warembo hao kuwa mabalozi wazuri wa kutangaza utalii na fursa mbali mbali zilizoko kwenye mkoa wa Manyara.
Afisa Masoko wa Kiwanda cha Mati Super Brands Limited Gwandumi Mpoma amesema kuwa kampuni hiyo itaendelea kudhamini mashindano hayo yenye lengo la kuibua vipaji vya vijana na kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii.
“Tumeridhishwa na uendeshaji wa mashindano haya ambayo yamezingatia misingi ya taratibu na kanuni na mshindi amepatikana kwa haki baada ya ushindano mkali” Alisema Gwandumi.
Social Plugin