Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

AFARIKI KWA KUANGUKIWA NA NG'OMBE KISIMANI AKIENDELEA KUCHIMBA


Mwanaume mmoja amefariki dunia baada ya kuangukiwa na ng'ombe kisimani akiendelea kuchimba katika kijiji cha Emukaba eneo bunge la Lurambi Kaunti ya Kakamega nchini Kenya.

Gordin Oningu Shivoko 46, alikuwa akichimba kisima alipoangukiwa na ngombe huyo ndani ya kisima hicho na kufariki dunia papo hapo.

Kulingana na walioshuhudia kisa hicho, wanasema ng'ombe huyo alikuwa kwa kikundi cha ng'ombe wengine waliokiwa wakipelekwa malishoni kabla ya kupita karibu na shimo hilo na kuanguka ndani.

"Ngombe alikuwa akisumbua, anakimbia huku na kule, mwendazake alikuwa ndani ya shimo, kwa bahati mbaya ngombe aliteleza na kuanguka ndani ya shimo hilo," alisema Mary Khasiala mmiliki wa boma alikokufia mwendazake.

Kwa usaidizi wa majirani, wakaazi walifaulu kumnasua mwendazake ila alithibitishwa amefariki dunia. "Wote wawili walikuwa wamefariki, ng'ombe alimwangukia mwendazake kwa sehemu ya nyuma na kumvunja vunja," alisema Tabitha Etemesi, mamake mwendazake.

Akithibitisha kisa hicho, naibu chifu wa eneo hilo Scolarstica Olando amesema mwili wa mwendazake ulipelekwa kwenye chumba cha kuhifadhi maiti ya hospitali ya Kakamega huku akiwaonya wakaazi dhidi ya kufanya kazi bila kuchukua tahadhari.

Hata hivyo kulingana na mila na tamaduni ya jamii ya mwendazake, ng'ombe huyo atafanyiwa tambiko kuwaepusha waliosalia dhidi ya kupatwa na maafa sampuli hiyo.

"Kulingana na jamii ya watsotso, ng'ombe huyo atakatwa katwa akiwa na ngozi na nyama yake kugawiwa majirani, jamii hairuhusiwi kuila nyama hiyo," Gilbert Mwakali alisema.

Chanzo - Tuko News

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com