Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

CHIFU MAZENGO AMVAA POLEPOLE KUBEZA MACHIFU "WATANZANIA WANAPASWA KUHESHIMU MILA NA DESTURI"


Chifu Mkuu Kanda ya kati Henry Mtemi Mazengo II

Na Dotto Kwilasa-Malunde 1 Blog- DODOMA.

CHIFU Mkuu kanda ya Kati Henry Mtemi Mazengo II amewataka watanzania kuheshimu mila na desturi za kitanzania kwa kuwa zina mchango mkubwa katika jamii na kwamba endapo zitaenziwa zitasaidia kuwepo kwa heshima ya haki za binadamu .

Mazengo ameyasema hayo leo Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni siku chache kupita tangu Mbunge wa kuteuliwa Humphrey Polepole kutoa kauli tata ya kuubeza utawala wa kichifu na kusema kuwa machifu hawana lolote. 

Amesema  wakati mwingine jamii hutumia haki za kitamaduni kama kisingizio cha kukandamiza wengine au kubinya haki zingine za binadamu katika jamii jambo ambalo si kweli.

"Zamani tulikuwa na utawala wa machifu, masultani na wafalme ili kuhakikisha watawala wanafanya kazi zao sawasawa himaya zilikuwa na vyombo vyake: majeshi, usalama, elimu, sanaa vyote hivi vilihakikisha masilahi ya uchumi na usalama wa raia,utaratibu ni huo huo hata zama hizo,tunaomba utamaduni uheshimiwe,"amesema Chifu Mazengo.

Amesema  suala la Mbunge huyo  wa kuteuliwa kusema utawala wa Machifu si lolote si chochote linaleta ukabila na mgawanyo  katika jamii wakati halina mashiko hivyo kutaka kila mtu kwa nafasi yake kulikemea.

"Taarifa hizi zinaligawa taifa na likichukuliwa kimzaha mzaha litarudisha chuki za ukabila,si SW la kulikalia kimya hata kidogo lazima tulikemee,"anasisitiza

Mbali na hayo ameeleza kuwa utawala wa kichifu hauna nia mbaya kwa taifa bali kuhakikisha jamii inakaa kwenye mstari na kuisaidia jamii kuepuka kwenda kinyume na utaratibu wa Mila na desturi.

"Polepole anapaswa kufahamu kuwa machifu tuna umoja wetu ambao unaisaidia Serikali kuhifadhi Mila zetu kwa vizazi vijavyo na ndio maana serikali inatambua na kuthamini mchango wetu,"amesema.

Aidha,Chifu Mazengo amesema ni muhimu kwa watanzania wote kuungana kwa pamoja kulinda amani ya Tanzania si kukaa na kushabikia kauli zinazoleta  mkanganyiko katika jamii.

Katika hatua nyingine ,Chifu Mazengo ameshauri viongozi mbalimbali kuwa mstari wa mbele  kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhi Hassan kukemea vitendo viovu mara vinapotokea bila kusubiri Rais aongee.

"Kabla ya wakoloni, tulikuwa na namna zetu za kuendesha mambo,sasa mambo yamebadilika sisi machifu tunabaki kwenye nafasi yetu lakini Kuna Viongozi wengine wanapaswa kusimama na kukemea haya maovu,"amesisitiza.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com