Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BENKI YA CRDB YATANGAZA UFADHILI WA MASOMO WA SH. MILIONI 10 KWA WACHEZAJI 10 BORA CRDB BANK TAIFA CUP

Benki ya CRDB imetangaza ufadhili wa masomo wa Shilingi Milioni 10 kwa wachezaji 10 bora wa mashindano ya taifa ya mpira wa kikapu “CRDB Bank Taifa Cup” 2021 katika hafla iliyoonyeshwa mubashara kupitia chaneli ya michezo ya AzamTV.

Akizungumza katika hafla ya kutangaza ufadhili huo, Meneja Mwandamizi wa Uwekezaji katika Jamii Benki ya CRDB, Joycelean Makule amesema ufadhili huo wa masomo kwa wachezaji ni muendelezo wa jitihada za Benki ya CRDB katika kuwawezesha vijana wa kitanzania kupitia michezo.

Joycelean alisema Benki hiyo kupitia sera yake ya Uwezeshaji katika Jamii (CSI Policy) imekuwa ikiwekeza katika michezo ya vijana kwa kuamini kuwa inasidia kuongeza ushiriki wao katika shughuli mbalimbali ikwamo elimu ili kusaidia kuwajenga kwa ajili ya maisha ya baadae.
“Katika CRDB Bank Taifa Cup wapo vijana wengi ambao bado wapo masomoni katika ngazi mbalimbali. Hivyo Benki iliona ni vyema kuambatanisha suala la elimu na michezo kwa kutoa ufadhili wa masomo vijana ambao wameonyesha uwezo mkubwa katika mashindano ya CRDB Bank Taifa Cup,” alisema Joycelean.

Akizungumzia kuhusu msukumo uliopelekea Benki hiyo kudhamini masomo ya wachezaji wa mpira wa kikapu Joycelean alisema mchezo wa mpira wa kikapu umekuwa haupewi sana kipaumbele kulinganisha na michezo mingine, hivyo kupelekea kuwakatisha tamaa vijana wengi ambao wamekuwa wakionyesha vipaji katika mchezo huo.
“Baada ya mchakato mrefu wa kufanya tathimini ya uwezo uliooneshwa na vijana pamoja na kufatilia taarifa zao za kielimu kwa kushirikiana na Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), tumefanikiwa kukamilisha zoezi hilo na leo tupo hapa kwa ajili ya kutangaza vijana waliofanikiwa kupata nafasi hizo za ufadhili wa masomo kwa mwaka 2021/2022,” alisema Joycelean ikibainisha.

Huu ni mwaka wa pili kwa Benki ya CRDB kutoa ufadhili wa masomo kwa wachezaji bora wa mchezo wa mpira wa kikapu kupitia CRDB Bank Taifa Cup. Mwaka jana benki hiyo ilitoa ufadhili wa masomo wa jumla ya shilingi milioni 50 kwa vijana 25. “Tunajivunia kuendelea kutoa ufadhili wa masomo kwa vijana kupitia mchezo huu kwani tunaamini utasaidia kufikia ndoto zao kupitia elimu,” aliongezea Joycelean.
Akizungumza kwa niaba ya vijana waliopata ufadhili wa masomo, mchezaji wa timu ya wanawake ya mpira wa kikapu mkoa wa Kilimanjaro Jesca Mbowe ambaye anasoma katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) shahada ya usimamizi wa utalii ameishukuru Benki ya CRDB kwa ufadhili huo, huku akisema utakuwa chachu kwao kusoma kwa bidii ili kufikia malengo yao.

Kwaupande wake Makamu wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania, Rwehabura Balongo ameishukuru Benki ya CRDB kwa kuendelea kuwekeza katika mpira wa kikapu huku akisema udhamini huo wa masomo utakwenda kuleta hamasa zaidi kwa vijana wengi kushiriki katika mchezo huo.
Balongo aliishukuru pia Benki ya CRDB kwa kuendelea kuwa mdhamini wa mashindano ya taifa ya mpira wa kikapu ambapo tokea benki hiyo ianze kushirikiana na TBF kumekuwa na mwamko mkubwa katika mchezo huo. Benki ya CRDB mwaka jana iliongeza udhamini katika Taifa Cup kufikia shilingi 300 ambapo timu 36 za mpira wa kikapu kwa upande wa wanaume na wanawake zilichuana vikali.

Timu za wanawake na wananume za mpira wa kikapu mkoa wa Dar es Salaam ziliibuka kidedea katika mashindano hayo yaliyofanyika katika viwanja vya Chinangali Dodoma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com