*************
Na John Mapepele
Mweyekiti wa Kikao cha Kamati ya Makatibu Wakuu wa Wizara zinazoshughulikia michezo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dkt. Hassan Abbasi amesema maafisa udhibiti ubora watakiwa kupima na kuwasilisha taarifa za ufundishaji wa somo la michezo nchini ili kupata tathimini ya maendeleo ya michezo nchini.
Akizungumza kwenye kikao cha Makatibu Wakuu wa Kamati hiyo iliyojumuisha Wizara yake, TAMISEMI na Wizara yenye dhamana ya Elimu leo Februari, 2,2022 jijini Dodoma amesema Kamati yake imekamilisha kazi iliyotolewa kufuatia maelekezo aliyoyatoa hivi karibuni Waziri wa TAMISEMI Mhe. Innocent Bashungwa ya kutaka Wizara hizo zikutane kuanzia ngazi za Wataalam, Makatibu Wakuu na baadaye Mawaziri ili kujadili mikakati ya kuendeleza michezo kama Taifa.
Amesema miongoni mwa masuala yatakayowasilishwa kwenye ngazi ya Mawaziri baada ya kikao hicho ni pamoja na Mkakati wa Utoaji wa Elimu kwa michezo shuleni ambao una malengo saba ambayo ni kuongeza idadi ya walimu wa somo la PE katika shule za Msingi na Sekondari ili kufikia uwiano wa shule 1 na mwalimu 1 wa masomo ya PE ifikapo 2025.
Malengo mengine ya mkakati huo ni kuteua shule tatu za michezo kwa Shule za Msingi na Sekondari katika kila Halmashauri,kuboresha miundoimbinu ya michezo katika shule 18152 za Msingi, 5143 za Sekondari na vyuo 36 vya ualimu na Michezo ifikapo 2025, kuimarisha ugharimiaji wa michezo katika shule na vyuo nchini kwa mwaka 2022, kutumia fursa ya ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika shule za Msingi na Sekondari na vyuo kwa maendeleo ya wanamichezo.
Pia kufanya tathimini ya ufundishaji na ujifunzaji wa somo la Elimu kwa Michezo kuanzia Elimu ya Awali hadi Sekondari na Kutenga, kujenga na kuboresha Miundombinu ya Michezo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ifikapo 2025.
Aidha ameongeza kuwa hoja nyingine inayotarajiwa kuwasilishwa kwenye kikao cha Mawaziri ni ya kufanya marekebisho ya mitaala ya Chuo cha Michezo cha Malya ili kiweze kuongeza masomo kadhaa ya kufundishia kwenye shule za misingi na Sekondari.
Dkt Abbasi amefafanua kwamba orodha ya shule teule za michezo 56 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo zitawasilishwa katika kikao hicho pamoja na mpango wote wa maboresho ya Shule za Sekondari za Tabora Wavulana na Wasichana kwa ajili ya mashindano ya UMISSETA na UMISHUMTA ya mwaka huu.
Katika kikao hicho mwenyekiti Dkt. Abbasi pia aliambatana na Naibu Katibu Mkuu wake Saidi Yakubu, Wakurugenzi wa Idara ya Michezo na Mtendaji Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa.
Social Plugin