GEKUL AWAFUNDA WASANII

 

****************

Na. John Mapepele

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Pauline Gekul amewataka wasanii kuendelea kuboresha kazi zao ili waweze kunufaika nazo.

Hayo ameyasema leo Februari 22, 2022 kwenye Ukumbi wa Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na wasanii kutoka Umoja wa Wasanii Wanawake Tanzania (UWAWATA) na kuutaka umoja huo kuwa mfano wa kuzingatia maadili kwa wasanii wanawake hapa nchini.

Mhe. Gekul amelielekeza Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kushirikiana na umoja huo kutafuta masoko ya kazi hizo.

Ameielekeza Idara ya Maendeleo ya Sanaa kwa kushirikiana na Taasisi zilizo chini ya Idara hiyo za BASATA, TaSUBa na Bodi ya Filamu kuandaa mpango wa mafunzo maalum ili kuwajengea uwezo wasanii kwa gharama nafuu.

Pia amewataka wanawake kuunda vikundi vidogo vidogo na kwenda Halmashauri ili kupata fedha zisizokuwa na riba zinazotolewa kwa ajili ya wanawake.

Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kupitia Mfuko wa Utamaduni na Sanaa na kutoa wito kwa wasanii kuchangamkia fedha hizo. Pia amelielekeza BASATA kusajili umoja huu mara moja.

Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania, Dkt. Kiagho Kilonzo ametoa wito kwa UWAWATA kusajili kikundi hicho au msanii mmoja mmoja ili waweze kutambulika na kunufaika na kazi zao.

Aidha, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Bakari Gaima amefafanua kuwa tayari Serikali imeshatengeneza mifumo ya kielektroniki ambayo wasanii wanaweza kujisajili wakiwa mahali popote duniani.

Mwenyekiti wa Umoja huo, Hidaya Njaidi ameiomba Serikali kuendelea kuwatumia Wasanii wanawake katika kampeni mbalimbali za maendeleo.

Njaidi pia ameiomba Serikali kuandaa Tamasha la Wasanii Wanaweke ili kusaidia kukuza vipaji vya wasanii wachanga na amempongeza Mhe. Rais kwa kushiriki kutengeneza Filamu ya Royal Tour ambayo itaitangaza Tanzania duniani.

Mhe. Gekul ametumia nafasi hii kuwakaribisha wasanii wa UWAWATA kushiriki kwenye tamasha kubwa la kihistoria la Muziki wa Serengeti litakalifanyika Machi 12, 2022 jijini Dodoma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post