Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HALMASHAURI YA JIJI LA DODOMA NA KASI YA MIKOPO KWA WAJASIRIAMALI KUCHOCHEA UCHUMI


Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru akiongea na wajasiriamali wakati wa makabidhiano ya mikopo ambayo imetajwa kuwanufaisha kiuchumi.
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri akisisitiza jambo kwenye hafla ya makabidhiano ya mikopo kwa wajasiriamali ili kuchochea kasi ya uchumi.
Baadhi ya wajasiriamali wanufaika wa mikopo iliyotolewa na Jiji la Dodoma ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi za Serikali katika kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja.
Wajasiriamali wakiwa wamebeba picha yenye mfano wa hundi ikiwa ni sehemu ya fedha walizokopeshwa na Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

Na Dotto Kwilasa-Malunde 1 Blog-DODOMA.

HALMASHAURI ya Jiji la Dodoma imekabidhi vifaa mbalimbali kwa vikundi vya ujasiriamali mkoani Dodoma ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi yake katika kuwatumikia wananchi ipasavyo kwa kuwasaidia kuzitambua fursa zao ili kuchochea kasi ya ukuaji uchumi nchini.


Mikopo hiyo ni pamoja na Lori aina ya fuso (Tan.7) kwa ajili ya kubebea mchanga na matofali,Pikipiki,na Bajaji ikiwa ni asilimia kumi ya mapato ya ndani ambayo yanatakiwa kurejeshwa kama mkopo kwa Vijana, Wanawake, na Watu Wenye Ulemavu.


Akiongea wakati wa makabidhiano ya mikopo hiyo leo Februari 3, 2022, mkuu wa Wilaya ya Dodoma Jabir Shekimweri amesema kuwa mikopo hiyo ni kwa ajili ya shughuli za viwanda,Guta 1,Lori moja la kubebea tofari na mchanga,fuso tani saba na mikopo kwa ajili ya biashasha ndogondogo, mikopo ya kilimo,mikopo ya mifugo na mikopo kwa ajili ya mama lishe na baba lishe.


Shekimweri amesema kuwa katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha halmashauri ya Jiji la Dodoma imeweza kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 8.87 kwa vikundi 78 vilivyokabidhiwa hundi leo.


Amesema juhudi hizi Kwa pamoja zinafaa zitumike katika kuwaletea maendeleo ya kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja,jamii inayomzunguka pamoja na taifa kwa ujumla kwa kutimiza nia ya serikali ya kukuza uchumi wa mtu na uchumi wa vitu.


Naye Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma Joseph Mafuru ameeleza kuwa hatua hiyo Itaibua fursa za uchumi kwa Vijana Mkoani hapa huku akiitaja hatua hiyo kuwa itasaidia katika mwelekeo wa kukuza sekta ya viwanda Mkoani Dodoma kama njia mojawapo ya kuchochea uchumi.


Amefafanua kuwa katika kutekeleza sera ya kutoa asilimia kumi katika makundi ya vijana,akina mama na makundi maalumu halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kipindi cha mwaka wa fedha imetoa jumla ya mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 8.87.


Mafuru pia ameeleza kuwa hadi sasa taarifa inaonesha kwamba shilingi 3,981,070,933.62 tu ndizo zimerejeshwa ambapo ni sawa na asilimia 44.9 ya kiasi cha mkopo kilichotolewa .


Kadhalika Mkurugenzi huyo wa Jiji la Dodoma amesema; "Katika mikopo iliyotolewa leo kwa upande wa vikundi 46 vya wanawake wamepata sh.395,000,000 ,vikundi 23 vya vijana wamepata sh.364,000,000 na vikundi 19 vya watu wenye ulemavu wamepata sh.58,400,000 na kufanya jumla ya vikundi 78 kupata jumla ya fedha sh.817,400,000,"amefafanua Mafuru.


Kutokana na umuhimu wa tukio hilo,Mbunge wa jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde ametumia nafasi hiyo kuvitaka vikundi vyote vilivyonufaika na mikopo hiyo kuitumia kwa lengo lililokusudiwa.


Mavunde ameimwagia sifa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa kutekelezwa kwa kiwango kikubwa takwa hilo la kisera la kutoa asilimia kumi ya mapato ya ndani kwa makundi hayo.


Naye Mwenyekiti wa kikundi cha Ilumbo Group ambacho kimenufaika na utaratibu huo Monica Masado amesema mikopo hiyo inawaoa chachu ya kujituma zaidi na kuondokana na utegemezi na kuweza kuinua maisha yao.


Akiongea kwa niaba ya wanufaika wa mikopo hiyo Masado ametumia nafasi hiyo kuwataka wakopaji wanaokopa mikopo hiyo kuwa waaminifu na kuhakikisha wanakopa na kurejesha kwa wakati.


"Lazima tuelewe tumekopa kujikwamua kiuchumi, wajasiriamali wenzangu lazima tuhakikishe tunafanya kazi na kufanya shughuli za maendeleo ,tusitumie fedha na vifaa hivi kwa makusidio tofauti kwani kwa kufanya hivyo tutawakwamisha wengine,"amesisitiza mjasiriamali huyo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com