Na Samirah Yusuph - Maswa
Maswa. Maafisa ugani wa kilimo cha pamba hai wanao wasimamia wakulima katika maeneo yao wamepewa mbinu za kudhibiti visumbufu pamoja na magugu katika zao la pamba hususani magugu, wadudu na magonjwa zinazoendana na masharti na miiko ya kilimo hicho.
Mafunzo hayo yametolewa kwa maafisa ugani 100 na kufungwa leo Februari 23,2022 wilaya ya Maswa mkoani Simiyu na Mshauri mzalishaji wa mazao ya kilimo hai nchini Leonard Mtama, yakiwa na lengo la kuwawezesha maafisa ugani kuwasimamia wakulima wanaozalisha pamba hai katika kutumia mbinu za kilimo hai kama zinavyoelekezwa katika kanuni za kilimo hai za kitaifa na kimataifa kulingana na soko linavyohitaji.
Amesema matarajio ya mafunzo haya ni kuwa uzalishaji wa pamba hai utaongezeka nchini baada ya kuwa wakulima wamepata elimu stahiki ya kilimo hai na hivyo itasababisha kuinua pato la mkulima mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
"Kilimo hai kinalenga kuzuia wadudu waharibifu na sio kupambana na wadudu ndio sababu ya kuanza kulinda mimea ya pamba tangu ikiwa michanga ili isishambuliwe na wadudu iweze kutoa matunda ikiwa katika hali nzuri",amesema Mtama.
Uzalishaji wa pamba hai nchini umeongezeka ambapo msimu wa kilimo 2020/21 Tanzania ilizalisha 5% pamba hai duniani ikishika nafasi ya tano na ikiwa ni nchi ya kwanza afrika kwa uzalishaji wa pamba hai.
Mkoa wa Simiyu ulizalisha pamba hai kilo milioni 9.2 na kati ya hizo kilo milioni 1.7 ilizalishwa wilaya ya Maswa.
Ambapo afisa mradi wa kilimo cha pamba hai kutoka kampuni ya SM holdings Majira Mayala amesema ili kuongeza tija kalika kilimo cha pamba hai kampuni hiyo imeajiri maafisa ugani 80 ambapo kila kijiji kinahudumiwa na maafisa ugani wawili.
"Lengo la kuweka nguvu nyingi katika kilimo cha pamba hai ni kuhakikisha wakulima wanapata uelewa wa kanuni za kilimo cha pamba hai ili kuongeza uzalishaji wa pamba hai yenye vigezo", amesema Mayala.
Kwa upande wa maafisa ugani wa serikali Faustine Petro na wamesema baada ya mafunzo haya wamebeba jukumu la kuhakikisha mkulima anainuka ki uchumi kupitia kilimo kwa sababu watakwenda kufundisha kilimo chenye tija.
"Lengo ni kuhakikisha mkulima analima kilimo chenye tija na anapata faida kwa sababu soko la pamba hai ni kubwa hivyo kwa kuzingatia kanuni za kilimo mkulima atazalisha pamba inayohitajika zaidi sokoni", amesema Faustine.
Akifunga mafunzo hayo mkuu wa wilaya ya Maswa Aswege Kaminyoge amewataka maafisa ugani waliopata mafunzo kwenda kutoa elimu kwa wakulima wote bila kuchagua wale wanaolima pamba hai kwa sababu wakulima wengine ni wakulima watarajiwa wa kilimo hicho.
"Maafisa ugani wanapokuwa kwenye maeneo yao wanaweza kufanya kazi ya Ushauri kwa wakulima ambao hawalimi kilimo cha pamba hai, wakulima watakapo pata elimu ya kutosha watalima, lengo ni kuongeza uzalishaji wa pamba hii",amesema
Amesema kuwa kwa kufanya hivyo kutawasaidia wakulima mmoja mmoja kuongeza uzalishaji wa zao hilo katika hekari moja na kujiongezea kipato sambamba na wilaya hiyo kufikia malengo ya kuzalisha tani za zao la pamba zipatazo 130,000 katika msimu huu wa kilimo.