Madaktari nchini Uganda wamethibitisha kuwa mwanamke Judith Nakintu mwenye umri wa miaka 38 aliyekuwa akifanya kazi za ndani nchini Saudi Arabia, aliondolewa figo yake ya kulia bila ridhaa yake na mwajiri wake na siyo ajali ya gari kama ilivyoarifiwa awali.
Wizara ya Mambo ya Ndani nchini humo, imethibitisha hilo baada ya kupewa ripoti ya uchunguzi kutoka Hospitali Kuu ya Taifa ya Mulago.
Kufuatia taarifa hizo za uchunguzi, sasa familia ya mwanamke huyo inaiomba serikali kusimamia suala hilo hadi haki itakapopatikana.
Judith mwenye watoto watano alichukuliwa na Kampuni ya Nile Treasure Gate mnamo mwaka 2019 kwa ajili ya kwenda kufanya kazi za ndani huko Jeddah nchini Saudi Arabia na wiki kadhaa zilizopita, alirejeshwa nyumbani akiwa amepata ulemavu kutokana na mateso aliyokuwa akipewa na mwajiri wake.
Social Plugin