Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAKAMU WA RAIS KUZINDUA SERA MPYA YA TAIFA YA MAZINGIRA


Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu Uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 unaotarajiwa kufanyika Februari 12, 2022 Jijini Dodoma.

 Na Dotto Kwilasa, Malunde 1 Blog- DODOMA

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa Sera Mpya ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 ambayo itazinduliwa tarehe 12 Februari, 2022 Jijini Dodoma. 


Hatua hii imekuja baada ya Ofisi ya Makamu wa Rais kukamilisha mchakato wa mapitio wa Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 1997 na kuandaa sera hiyo mpya ambayo imejumuisha masuala ya mazingira yaliyokuwemo katika Sera ya 1997 .

Hayo yamebainishwa leo Jijini Dodoma na Katibu Mkuu,Ofisi ya Makamu wa Rais-Muungano na Mazigira Mary Maganga na kufafanua kuwa Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 imeongeza wigo wa masuala na changamoto za mazingira zinazopaswa kufanyiwa kazi katika kipindi husika ili kuleta maendeleo endelevu.

 

"Sera mpya imezingatia changamoto mpya za kimazingira zinazoendelea kujitokeza kutokana na mabadiliko ya mifumo ya kiuchumi, kijamii na kimazingira yanayoendelea duniani, Serikali imeamua kuwa na Wiki ya Uzinduzi wa Sera  itakayoanza tarehe 07-12/02/2022 ambapo shughuli mbalimbali za hifadhi ya mazingira zitafanyika ikiwa ni sehemu ya masuala ya msingi yanayoelekezwa katika Sera mpya,"amesema.


Kadhalika  Maganga amesema kuwepo kwa shughuli hizo kutasaidia kurejesha hali ya asili ya mazingira iliyoharibika kutokana na shughuli za kibinadamu kwa kuwa na zoezi la upandaji miti,kutakuwa na shughuli za usafi wa mazingira zinazolenga kuboresha afya ya jamii na elimu ya utenganishaji taka kwa ajili ya udhibiti wa taka ngumu na kuwezesha urejelezaji wa taka kwenye bidhaa na huduma mbalimbali. 


"Kwa muktadha huo, shughuli zitakazotekelezwa katika wiki ya uzinduzi huo ni pamoja na upandaji miti Jijini Dodoma katika maeneo ya  Medeli,siku ya tarehe 07/02/2022 Iyumbu,siku ya tarehe 08/02/2022Isern,siku ya tarehe 09/02/2022 maeneo ya barabara inayoanzia Chimwaga, Chuo Kikuu cha Dodoma kuelekea barabara ya Dodoma Dar es Salaam (siku ya tarehe 12/02/2022.


Aidha kutakuwa na shughuli za kufanya usafi pembezoni mwa barabara inayoanzia Shule ya Martin Luther hadi Wajenzi kupitia Nzuguni, Illazo, Ipagala na Area C;Kutoa elimu kuhusu utenganishaji wa taka na kufanya Usafi katika soko la Changombe; Utoaji wa Elimu ya Mazingira kwa wananchi na wadau kupita vyombo vya habari,"amefafanua Maganga.


Pamoja na hayo Katibu Mkuu huyo ameeleza kuwa shughuli zote zimepangwa kuanza saa 1.00 hadi saa 3.00 kamili asubuhi huku akitumia nafasi hiyo kuwaalika wadau wote wa mazingira nchini hususan wa Mkoa wa Dodoma na viunga vyake kushiriki katika hafla hiyo ya uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Mazingira pamoja na shughuli zote zitakazofanyika katika Wiki ya Uzinduzi wa Sera. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com