Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAMBO YA KUFANYA ENDAPO SIMU YAKO IKILOWA AU KUINGIA KWENYE MAJI


Ulikuwa umeishika vibaya na ikakuponyoka na kuangukia kwenye beseni..au kwenye dimbwi la maji… au kwenye sehemu ya kuogelewa (Pool).. Hizo ni baadhi tuu ya maeneo ambayo yanaweza sababisha simu au tableti yako kukutana na maji. Jambo ambalo linaweza sababisha kufa kwa kifaa chako cha bei nono!

Mara nyingi jambo la kwanza atakalofanya mtu ni kuhangaika kufuta maji hayo mara moja…. iwe kwa kutumia nguo yake, au chochote kile cha karibu. Ila je ni sahihi? HAPANA!

Hatua ya 1:

Itoe mara moja kwenye maji. Inavyozidi kukaa kwenye maji muda mrefo ndivyo uwezekano wa kupona katika janga hili unakuwa mdogo zaidi. Imedondoka kwenye choo? Hapo itakubidi ufanye maamuzi ya haraka kama utaichomoa haraka au uisahau kabisa. Utafanya nini?

Hatua ya 2:

Bila kupoteza muda izime mara moja! Na kama ni simu yenye eneo la kutoa betri basi usitumie switchi yake kuzimia, bali toa betri mara moja. USIJARIBU KUBONYEZA KINGINE CHOCHOTE, ONDOA BETRI. Na kama ni tableti au simu za iPhone ambazo hazina sehemu za kutolea betri bofya eneo la kuzimia mara moja.

LENGO: Ni kuzima simu au tableti hiyo kabla hakujatokea shoti ya aina yeyote, kama simu imeingia maji alafu ukaifuta na kuanza kujaribu kuichezea kwa kubofya unaweza sababisha shoti inayoweza ikaiua simu yako mara moja.

Hatua ya 3:

Ifute taratibu. Kwa kutumia kitu kama taulo lililo kavu, angalia kwa ukaribu maeneo kama vile ya kuweka waya wa ‘earphones’, hakukisha pameacha kutoa maji. Puliza maeneo ya matundu kuhakikisha maji yameisha kabisa ndani. Pia toa vitu kama vile kadi ya laini, memori kadi na betri, kava, vikaushe pia.

Usitumie njia za ajabu kama vile kuiweka kwenye oveni ili kuikausha…joto la oveni ni kali sana utaua simu yako. 🙂

Hatua ya 4:

Njia A: Unavijua vipakti flani hivi vidogo vinakuwaga kwenye viatu vipya? Vinaitwa “silica gel packets”, ndani yake inavidonge vidogo vya Silica. Kama unavyo au unaweza kuvipata basi chukua mfuko wa plastiki unaoweza kuufunga kuzuia hewa, weka simu yako na vipakti hivyo katika mfuko huo kisha ufunge.

Vidonge hivi vinasifa ya kunyonya unyevu nyevu, kuweka sehemu moja na kuvifungia na simu yako kutahakikisha unyevu nyevu uliopo kwenye simu yako kunyonywa na vidonge hivyo.

Njia B: Kama njia A haiwezekani basi fuata njia hii, zungushia simu yako kwenye tishu (Toilet Paper/Napkins) kisha iweke kwenye chombo ulichoweka mchele wa kutosha kuifunika kabisa. Mchele unasifa ya kunyonya unyevunyevu kama vile kwenye njia A. Unazungushia tishu ili kuondoa uwezekano wa simu yako kuingiwa na vumbi la mchele.
Ila njia A, ndiyo bora zaidi katika hizi mbili. Ile inawahisha kukauka kwa haraka zaidi ukilinganisha na njia ya kutumia mchele. Kama hauna vidonge hivi basi hakikisha kuanzia sasa wewe au jirani/rafiki yako akinunua viatu vipya tuu uchukue na huifadhi vidonge hivi kwani uwezi kujua lini unaweza kuviitaji. Na kumbuka huwa pia unaweza kuvikuta katika bidhaa nyingine mpya, kama vile nguo au ata vitu vya kielektroniki, kuanzia sasa ukivipata vihifadhi katika mfuko au chombo cha plastiki kisichoruhusu hewa kabisa.

Hatua ya 5:

Baada ya kufanya tulichoongelea katika hatua ya 4 itakubidi usibiri takribani masaa 32 hadi 72, hapa kipimo ni chako wewe. Kama ililowa kidogo tuu basi masaa 32 yatatosha kabisa, ila kama ililowa sana, basi hakikisha ikae masaa 72. TUNAJUA UTAKUWA UNAHAMU YA KUIWASHA AU KUITOA KABLA, ILA KUMBUKA NI MUHIMU IKAUKE NDANI KABISA, Hivyo vumilia.

Hatua ya 6:

Tunajua baada ya hatua hizo zote utakuwa unasubiria kwa hamu kuiwasha tena. Hadi sasa itakuwa imekauka vizuri ndani, ukiiwasha tunategemea itawaka bila tatizo lolote kama ulifuata hatua zote kwa usahihi.

MAMBO MUHIMU YA KUFAHAMU
Njia hii inategemea bahati na uharaka wako katika kuondoa simu na kuizima baada ya kuwa katika maji. Kitu muhimu na kuweza kuzima simu au tableti hiyo kabla shoti haijatokea ndani yake

Ata kama itawaka vizuri na kuweza kufanya kazi kama kawaida kuna uwezekano mkubwa sana simu hiyo kuanza kutofanya kazi vizuri baada ya kipindi kirefu kama vile mwaka mmoja hivi kutokana na madhara ya kuingiwa na maji. Kuna vitu ndani yake huwa havitakiwi kukutana na maji kabisa. Hivyo ata kama itawaka na kuanza kufanya kazi kama kawaida anza kujiandaa kununua simu nyingine.

Kama simu yako ilikuwa bado ya Dhamana, yaani Warranty basi jua dhamana hiyo imevunjika rasmi. Simu janja nyingi za kisasa zinazouzwa zikiwa chini ya dhamana ya mwaka au miaka miwili zikikupa uwezo wa kuzirudisha na kupewa mpya n.k kutoka pale uliponunua huwa dhamana hizo zinafutwa kama simu iliingia maji. Na wameweka teknolojia spesheli (water indicator) ndani ya simu hizo ambapo kama simu au tableti zikilowa huwa wakifungua ndani wanatambua.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com