MAMBO YA KUZINGATIA UNAPOTUMIA UBER, BOLT,TAXIFY


 Abiria wa Uber akiwa safarini katika kiti cha nyuma. Picha ya Mtandao.
**
Matumizi ya teknolojia katika uchukuzi yanazidi kuongezeka kwa kasi nchini jambo linaloonyesha matumaini chanya namna ya kuzinyonya fursa za kidijitali

Tayari kuna kampuni kubwa za Uber, Bolt na Taxify zinazotoa huduma za uchukuzi jijini Dar es Salaam kwa watumiaji kuomba taxi kwa kutumia programu ya simu (App). Kila kitu katika mchakato wa kukodi taxi kinafanywa na app.

App hizo mbili zinazidi kuwa maarufu kila uchwao katika jiji hili lenye tatizo la usafiri kutokana na uwepo wa foleni kubwa na uhaba wa daladala hasa nyakati za mahitaji ya juu ya asubuhi na jioni licha ya kuwepo mabasi ya mwendokasi na huduma za treni.

Kutokana na shuruba hizo, Uber, Bolt and Taxify zimekuwa wakombozi kwa kuwa zinatoa usafiri kwa bei nafuu ikiwa ni nusu ya nauli za taxi za kawaida. Kati ya hizo, Uber imekuwa maarufu kwa sababu ndiyo ilikuwa ya kwanza kufika mwaka mmoja na nusu uliopita.

Hata wakati wana Dar es Salaam wengi wakiendelea kutumia Uber au Taxify kupata suluhu ya matatizo ya usafiri, kuna mambo ya msingi ya kuzingatia ili kuzuia gharama za ziada zisizo za lazima, kuongeza usalama na kulinda heshima yako na madereva wa magari hayo.

Yafuatayo ni baadhi ya mambo ya kuzingatia unapotumia Uber, Bolt Taxify au usafiri unaofanana nao.


Soma masharti na vigezo vya huduma

Kabla ya kuanza kutumia app yoyote ile iwe ya usafiri au mtandao wa kijamii ni bora usome na kuelewa masharti na vigezo vya huduma husika. Kukubali masharti hayo ni kuingia mkataba na mtoa huduma kuwajibika na kunufaika na sera za faragha na gharama zozote zitakazojitokeza wakati wa matumizi.

Kwa mfano, ukiomba Uber na dereva akafika na kuanza kukusubiri hadi zaidi ya dakika 10 kisha ukaihirisha safari utachajiwa gharama za ziada zitakazokuwa deni. Deni hilo litajumuishwa utakapoomba usafiri huo hapo baadaye.


Jipange na safari yako

Unapotumia Uber ni vyema ukajua eneo hilo unaloenda kwa kuchagua kwenye ramani kama jina lake lipo. Kama eneo hilo halijajumuishwa kwenye ramani basi jitahidi kutafuta kituo cha karibu kabisa au kuweka alama ya uendapo karibu na utakaposhukia ili kujua gharama halisi za usafiri ili kuzuia usumbufu wa kubishana na dereva.

Kwa wale ambao app hujiweka eneo la mwisho ulilokuwepo, ni vyema kuhakikisha sehemu unayoomba uchukuliwe ni pale ulipo kwa kuangalia kwenye ramani huku GPS ikiwa imewashwa. Kuna wakati unaita Uber alama ya ulipo ikiwa kwenye eneo la mwisho ulilokuwepo awali au ambalo ni tofauti kabisa na ulipo jambo linaloleta usumbufu kwa madereva na wanaweza kukuripoti Uber kwa usumbufu.

Jitahidi kuwa na nauli zaidi ya makadirio unayoonyeshwa

Ni kawaida kupewa makadirio ya nauli ya safari yako ndani ya Uber. Hata hivyo, kuna wakati nauli hiyo huzidi makadirio baada ya safari kutokana na sababu mbalimbali kama foleni au umbali ulioeleza kuwa zaidi ya ule uliosafiri. Kuzuia mvutano na dereva ni vyema ukawa na fedha ambayo inazidi makadirio ya nauli uliyoonyeshwa ambayo wakati mwingine huwa pungufu.


Pendelea kukaa kiti cha nyuma

Japo Uber huaminika kwa usalama bado ni vyema kujihami hasa pale utakapokuwa pekee yako. Uber wenyewe wanashauri ukae kiti cha nyuma kwa usalama ikitokea dharura iwe ni rahisi kutoka tofauti na kiti cha mbele ambacho upande mmoja umezuiwa na dereva. Mambo ya kuonyesha umepiga kishoka kiti cha mbele kama bosi kwenye Uber kuna wakati mwingine yanagharimu.


Tumia lugha nzuri uwapo ndani ya Uber

Baadhi ya watu hukosa lugha ya staha wanapokuwa na Uber. Dereva wa Uber anastahili heshima kama walivyo madereva wengine wa taxi na ndiyo ustaarabu wa mwanadamu. Iwapo utatoa lugha za kuudhi dereva atakupa nyota chache ikionyesha kuwa hakuridhishwa na wewe na anaweza kukuripoti kwa maneno yako na matokeo yake kuna wakati kila ukiomba gari utakuwa hupati huduma.


Acha ubosi usio wa lazima

Kuna wakati mtu akikodi Uber anajiona kama amenunua gari lote na kutaka kufanya kila kitu ndani ya gari. “Ongeza sauti ya mziki” “weka reggae”, “punguza AC”, “simama kidogo nitazame kitu”. Jaribu kuwa mstaarabu kwenye gari la watu. “Mbona kwenye daladala husemi yote hayo? Ni Dhahiri unahitaji huduma bora lakini uombe ufanyiwe kwa ustaarabu.

Uber, Bolt na Taxify ni wakombozi kwa usafiri wa haraka na wa muda wote ila manufaa yataonekana zaidi iwapo wote madereva na abiria watazingatia taratibu muhimu ili kuongeza mahusiano na kukuza biashara.

Chanzo - NUKTA HABARI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post