Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAKUTANA NA NGO’s KANDA YA ZIWA KUPOKEA MAONI YA UANDAAJI WA MKAKATI WA UENDELEVU WA NGO's


Wadau mbalimbali wa mashirika yasiyo ya kiserikali wakiwa kwenye mkutano wa kutoa maoni ya uandaaji wa mkakati wa uhimilifu na uendelevu wa mashirika katika ukumbi wa Nyerere uliopo Gold Crest Jijini Mwanza

Na Hellen Mtereko, Mwanza
Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na makundi maalum kupitia ofisi ya msajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la mashirika yasiyo ya kiserikali (NaCoNGO) wamefanya Mkutano wa wadau wa sekta ya NGOs Kanda ya Ziwa.

Mkutano huo umefanyika leo Jumatano Februari 23,2021 katika ukumbi wa Nyerere uliopo Gold Crest Jijini Mwanza.

Mkutano huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu  ambayo aliyatoa Septemba 30,2021 alipokutana na mashirika yasiyo ya kiserikali katika mkutano wao wa mwaka na baada ya kikao alitoa maagizo kwa wizara hiyo kufanya utafiti na kuona namna nzuri ya kuweza kuyasaidia mashirika hayo kuondokana na hali ya utegemezi.


Lengo la mkutano huo ni kupokea maoni ya wadau mbalimbali kutoka katika mashirika yasiyo ya kiserikali,sekta binafsi juu ya uandaaji wa mkakati wa uhimilifu na uendelevu wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali.

Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi msaidizi katika usajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali, kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na makundi maalum, Mussa Sanganyo amesema kuwa katika kipindi cha ugonjwa wa mafua makali uliosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19) uliathiri mashirika mengi kutokana na kutegemea fedha za msaada kutoka nje.


Amesema mashirika mengi yalitetereka katika kutekeleza miradi iliyokuwepo na hata iliyokuwa imepangwa kuanzishwa ilishindikana, hivyo kutokana na changamoto hiyo Serikali iliwafumbua macho wizara inayosimamia mashirika kuanza kuwajengea uwezo wa kujiendesha wenyewe bila kutegemea msaada.


"Utekelezaji umeanzia kwa Kanda ya Ziwa ambapo kikao kimefanyika Mkoani Mwanza ila tutatembelea Kanda zote nchini kwa ajili ya kuwakutanisha mashirika yasiyo ya kiserikali ili watoe maoni ya nini kifanyike ili waweze kusimama wenyewe katika kutekeleza shughuli zao", amesema Sanganyo.

Mwenyekiti kamati maalumu ya mkakati wa uhimilifu na uendelevu wa mashirika yasiyo ya kiserikali, Nesia Mahenge amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa sana wa mashirika hayo kuanza kujiendesha yenyewe ili wawe na uhakika wa kutekeleza shughuli zao.

Amesema inapotokea mfadhili akasitisha ufadhili katika shirika husika wananchi wataathirika kwa kukosa zile huduma ambazo walikuwa wakizipata.

Naye Katibu Mkuu wa Baraza la mashirika yasiyo ya kiserikali (NaCoNGO), Revocatus Sono amesema kuwa njia ya kupata maoni ni pamoja na vikao mbalimbali ambavyo vitafanyika ili kuweza kuwa na mlengo mmoja wa kuyasaidia mashirika haya kuwa endelevu.


Kwaupande wake mratibu miradi kutoka Shirika la Emedo, Arthor Mgema ambaye ni mshiriki wa mkutano huo amesema kuwa kikao hicho kimefanyika wakati sahihi na kimewapa nafasi ya kutoa maoni na kujadili kwa pamoja ili kuweza kutengeneza mkakati wa Kitaifa ambao utawasaidia kuwa na mbinu mbadala wa kuendesha mashirika yao kuwa endelevu.
Nesia Mahenge Mwenyekiti kamati maalumu ya mkakati wa uhimilifu na endelevu wa mashirika yasiyo ya kiserikali akizungumza katika mkutano uliowakutanisha wadau wa Sekta ya NGOs kutoka kanda ya ziwa uliofanyika leo Februari 23,2022 Jijini Mwanza
Viongozi mbalimbali mbalimbali wakiwa kwenye mkutano wa kutoa maoni ya uandaaji wa mkakati wa uhimilifu na uendelevu wa mashirika yasiyo ya kiserikali leo hii Februari 23,2022
Wadau kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali wakiwa katika mkutano uliofanyika Leo hii Jijini Mwanza uliolenga kujadili na kutoa maoni ya uandaaji wa mkakati wa uhimilifu na uendelevu wa mashirika yasiyo ya kiserikali ulioandaliwa na Wizara ya maendeleo ya Jamii jinsia wanawake na makundi maalum kwakushirikiana na Baraza la Taifa la mashirika yasiyo ya kiserikali (NaCoNGO)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com