Wakili wa waleta rufani katika kesi ya jinai namba 105 iliyomtia hatiani aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, Mosses Mahuna, amedai kwamba ushahidi uliotolewa mahakamani haukutosheleza kuwatia hatiani washtakiwa kwa makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kutumia genge la uhalifu.
Pia amedai kwamba Jeshi la Polisi lilifanya makosa ya kutokumkamata haraka aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya, kwa madai ya kwamba alikuwa mteule wa Rais, hivyo walitakiwa kupewa kibali cha kumkamata.
Wakili huyo alitoa madai hayo jana wakati wa usikilizwaji wa rufani namba 129 ya Sabaya na wenzake wawili, mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Sedekia Kisanya.
Akiwasilisha hoja ya pili ya kupinga hukumu iliyotolewa mahakamani huko, Wakili Mahuna alidai kwamba utata mwingine katika hukumu hiyo umeonekana pale tukio limetokea na wahusika kuchelewa kukamatwa.
Alidai kwamba kwa mujibu wa shahidi wa saba katika shauri hilo, Inspekta Gwakisa Minga, hawakuwakamata washtakiwa hao hasa mshtakiwa wa kwanza, Sabaya, kwa kuwa alikuwa mteule wa Rais.
"Alikuja hapa mahakamani Inspekta Gwakisa Minga, alitueleza kwamba walichukua muda mrefu kumkamata Sabaya kwa kuwa alikuwa mteule wa Rais. Ilitakiwa wapewe kibali cha kumkamata. Je, swali letu ni kwamba kama mtu alikuwa jambazi wangesubiri kwa kipindi chote kupewa kibali?" Alidai Mahuna.
Wakili Mahuna alidai kwamba hoja ya 13 ya waleta rufani wanalalamika kwamba Mahakama ya Hakimu Mkazi, ilikosea kwa kuwa washtakiwa hao hawakutambuliwa kwa utaratibu na njia sahihi zinazotakiwa.
Kadhalika, alidai kwamba kwa mujibu wa shahidi wa pili wa mashtaka Hajirini Saad, alidai hakukuwa na silaha iliyotumika na Mahakama ya Hakimu Mkazi, ilitoa kosa hilo kutoka kwenye unyang’anyi wa silaha kwenda kwenye unyang’anyi wa kutumia genge.
"Hakuna ushahidi wowote unaothibitisha kuna kiasi cha fedha kiliibwa kwenye shtaka la kwanza kwa kuwa shahidi wa pili aliyetakiwa kuthibitisha hilo alisema hajui kiasi cha fedha kilichoibiwa dukani wala kumwona mtu aliyempiga.
"Shahidi wa sita wa mashtaka, Bakari Msangi, alitueleza hapa mahakamani akiwa kwenye gari wakati wakiondoka dukani, aliona fedha bando mbili za milioni moja moja zikiwa kwenye mfuko wa rangi ya kaki. Pia alidai wakiwa Tulia Lodge, Sabaya alimwonyesha bando moja la fedha huku akimwambia wewe mtoto wa kiswahili umeona hela?” alidai Mahuna.
Katika shtaka la tatu la uporaji wa simu na Sh.35,000 mali ya Ramadhani Ayubu, alidai kuwa shahidi huyo alishindwa kuthibitisha mahakamani kwamba aliibiwa fedha hizo na simu aina ya Tecno Pop 1.
"Mahakama ya Hakimu Mkazi ilipaswa kuwaachia huru katika shtaka hili kwa kuwa shahidi alishindwa kuthibitisha kwamba aliporwa fedha na kunyang’anywa simu yake na ushahidi haukutosha kuwatia hatiani kwa kosa la unyang’anyi kwa kutumia silaha,” aliendelea kudai.
Wakili mwingine wa waleta rufani, Majura Magafu, akizungumzia hoja ya tatu, alidai kwamba vielelezo vya ushahidi wa picha na barua iliyopelekwa maabara ya uchunguzi wa kielektroniki vimetengenezwa na vilipokewa mahakamani kinyume cha utaratibu.
Alidai kwamba mkata rufani wa tatu (Daniel Mbira), aliieleza mahakama kuwa siku ya tukio hakuwapo eneo la tukio na hakimu hakuzingatia ushahidi wake wakati akiandaa hukumu hiyo.
"Mahakama ilishindwa kutambua utaratibu wa gwaride la utambuzi ulivyofanyika na tunaona halikuwapo. Pia lilitakiwa kufanya kwa mshtakiwa wa kwanza na mpaka leo hii hakuna ushahidi kwamba washtakiwa wa pili na wa tatu hawakukamatwa na kuhojiwa na kuchukuliwa maelezo ya onyo.” Alidai.
Wakili wa mrufani wa pili, Sylvester Kahunduka, kwa pamoja akiwasilisha hoja ya saba, 10 na 14 za kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, alidai wameshindwa kuelewa kwamba mahakama ilimwamini shahidi yupi na sababu zipi kwa kuwa ushahidi uliotolewa unakinzana.
"Tunashindwa kuelewa kama tukio la kupora kwa kutumia silaha lilifanyika kwa kuwa ushahidi uliotolewa unakinzana na uliokuwa wa uongo. Hakimu angefanya uchambuzi wa kina wa ushahidi, angebaini dosari mbalimbali," alidai Wakili Kahunduka.
Wakili Kahunduka alidai kwamba mashahidi wa mashtaka wametia wasiwasi kwa ushahidi wao na kama hakimu angekuwa makini, angebaini dosari zilizojitokeza.