WATU wawili, Suzana Mtitu (38) na Kassim Kitamkanga (35) wakazi Makambako Mkoani Njombe wamekutwa wamefariki katika msitu wa Tanwat uliopo Njombe huku uchunguzi ukibainisha kuwa wameuawa na mganga wa Jadi baada ya watu hao waliokuwa wateja wake kubaini kwamba dawa za kuwa matajiri walizopewa hazijafanya kazi.
RPC wa Njombe, Hamis Issah amesema Jeshi la Polisi linamshikilia Mganga huyo wa kienyeji, Joseph Mgunda (41) Mkazi wa Sovi Kata ya Mtwango Wilayani Njombe kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo.
“Watu wengi wafanyabiashara huyu Mganga anawaambia ukipeleka hela anaziombea, baadaye zinaongezeka, sintofahamu iliyotokea kwa hawa watu wawili walipewa dawa tayari lakini wakaona matokeo hayaleti mafanikio wakaenda kumuuliza mganga mbona umetupa dawa ambayo haisaidii, Mganga huyo alishikwa na hofu na kushauriwa na ndugu zake kutekeleza mauaji hayo.
“Ndugu zake wakamwambia ukitaka usipate shida waue hawa watu na kweli watu watatu na yeye mwenyewe Mganga akiwa ni wanne wakatekeleza mauaji, mwanaume alikatwa mapanga sehemu za shavuni upande wa kulia na kushoto na kichwani na pia kapigwa rungu na kudondoka na mwanamke alipigwa rungu moja tu na kudondoka chini.
Kamanda Issah amesema watu wengine wanaoshikiliwa kwa tuhuma za mauaji hayo ni Andrew Vahuruka, Gadi Mwanzalila (36) na Kelvin Kilinge (29), Kamanda Issah ametoa wito kwa wananchi kutafuta pesa kwa juhudi za kufanya kazi na sio kutafuta utajiri kwa Waganga kwa kuwa hakuna utajiri unaoletwa na Waganga.
Social Plugin