MLINZI wa shule ya Winnings Spirit iliyopo eneo la Terati jijini Arusha, Issa Dinaiah (57) amekutwa ameuawa kwa kuchinjwa huku kichwa kikiwa hakipo.
Mwili wa mlinzi huyo umekutwa leo Jumatano Februari 2, 2022 asubuhi na wafanyakazi wa shule hiyo inayomilikiwa na Meya wa Jiji la Arusha, Maximilian Iranghe.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meya Iranghe amesema alipata taarifa za kifo cha mfanyakazi wake mmoja leo asubuhi na baada ya kufika eneo la tukio aliwakuta Polisi. Iranghe amesema bado chanzo na waliofanya mauaji haya hawajajulikana.
“Naomba kuwasiliana na Polisi ambao ndio wanaendelea na uchunguzi wa tukio hili mimi nimepigiwa simu na wafanyakazi na nimekuta tayari polisi wapo hapa” amesema.
Maofisa wa Jeshi la Polisi waliokuwa katika eneo la tukio wameeleza taarifa rasmi itatolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa baada ya uchunguzi wa awali kukamilika.
Social Plugin