Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Dkt. YONAZI : SERIKALI ITAENDELEA KUWALINDA WANANCHI WAKE DHIDI YA UHALIFU MTANDAONI

Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt.Jim Yonazi akifunga mafunzo ya siku tano yanayohusu usalama mtandaoni kwa wapelelezi na askari wa chumba cha mashtaka Jijini Dodoma.

Na Dotto Kwilasa-Malunde 1 Blog-DODOMA.

KATIBU Mkuu,Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi amesema  Serikali itaendelea kuwalinda wananchi wake kutokana na uhalifu wa mitandao ili kuhakikisha nchi inakuwa salama.

Dkt. Yonazi ameeleza hayo leo Jijini Dodoma wakati akifunga mafunzo ya siku tano yanayohusu usalama mtandaoni kwa wapelelezi na askari wa chumba cha mashtaka na kueleza kuwa jambo la usalama mtandao ni  muhimu  kutiliwa mkazo hasa katika zama hizi za kidigitali kwa kuwa uwepo wa usalama  katika matumizi ya mitandao ni sawa sawa na kuhakikishia dunia inakuwa salama.

Mbali na hayo amebainisha kuwa zaidi ya watu milioni 18 duniani ni watumiaji wa huduma ya mtandao (internet) idadi ambayo ni kubwa hivyo ni muhimu sana kuweka namna sahihi ya kulinda usalama wa watumiaji hao.

“Dunia imebadilika sana tofauti na ilivyokuwa zamani,hivi sasa masuala ya usalama na ulinzi yanategemea TEHAMA,wachafuzi nao wanapata fursa kuharibu kutumia Teknolojia hiyo kuvuruga amani,nawaomba mkaendelee kuboresha mbinu mlizojifunza hapa  kuhakikisha usalama katika matumizi ya mitandao unaboreshwa,hakikisheni mnaepusha  madhara ya matumizi mabovu ya mitandao,” amesema Dkt. Yonazi.

Amesema, kupitia mafunzo hayo ya siku tano,walinzi hao wa usalama mtandaoni wanapaswa kushirikiana katika hatua changamoto zote uhalifu mtandao na kwamba Kwa kufanya hivyo watadhihirisha namna ambavyo Tanzania imejipanga katika kuhakikisha matumizi ya mitandao yanakuwa salama.

"Tunaamini kuwa tunayo nchi inayojilinda ,tunao wananchi wanaotegemea sana ulinzi wa mtandao Ili waishi Kwa amani na kuendelea kufanya shughuli nyingine za uzalishaji bila woga,ni jukumu lenu kulinda usalama wa taifa hili kwa kuzuia uhalifu wowote wa mtandao,"amesema

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DCI) Camilius Wambura amesema Idara hiyo itahakikisha inaboresha mifumo ya kuhakiki uhalali wa taarifa zinazopitia kwenye mitandao ambayo imebuniwa na wataalam wa Teknolojia ya Habari nchini Ili kuzuia matumizi mabaya ya mitandao.

"Makosa ya mtandao yanakuwa mengi na kusababisha uvunjifu wa amani na kuharibu furaha Kwa watu wengine,kupitia mafunzo hayo yataleta matokeo chanya kutokana na mbinu mlizopata ili kukabiliana na uhalifu wa kimtandao kwani maarifa yatawasaidia katika kubadilishana taarifa,"amesema.

Kadhalika Wambura ametumia nafasi hiyo kuwataka wapelelezi hao pamoja na askari kuhakikisha wanazingatia misingi ya kazi na wito wa maadili ya kazi yao ikiwa ni pamoja na  kufanya  kazi kwa kushirikiana ili kuweza kufikia malengo.

"Nendeni mkahakikishe  mnafanya kazi kwa uadilifu na nidhamu katika utendaji kazi wenu kwani tabia za wachache zimekuwa zikiharibu taswira ya Jeshi jambo ambalo si jema,"amesisitiza.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com