Mwili wa aliyekuwa mkazi wa Kihonda Mizani, Mark Mkude (67) umelazimika kuzikwa katika kaburi mbili tofauti kutokana na awali kuzikwa katika kaburi lililoandaliwa kwa ajili ya kuzikwa mwili wa aliyekuwa mkazi wa Bigwa Soko Manispaa ya Morogoro, Gervas Chondomba (71).
Mkude na Chondomba wote walifariki Februari 9, 2022 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro huku ndugu wa Chondomba wakichukua mwili wa Mkude bila kugundua utofauti.
Mwili Mkude ambao umefukuliwa Februari Ijumaa 10, 2022 asubuhi umekaa kaburini siku moja baada ya kuzikwa siku ya Alhamisi na umezikwa tena jana jioni.
Akizungumza na wakati wa mazishi ya Gervas Chondoma, Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Bigwa Sokoni kata ya Kilakala mjini Morogoro, Justine Mkoba amesema mwili wa Chondoma uliachwa chumba cha kuhifadhia maiti na kuchukuliwa mwili ambao sio wao na kuuzika juzi kabla ya kuufukua siku ya jana.
“Majina yalichanganywa, jina la marehemu huyu amepewa yule na jina la yule amepewa huyu ndio moja ya tatizo lilianzia lakini marehemu hao sura na tofauti zao zilikuwa ndogo sana nafikiri limetokea hili kwa sababu ya kukosa umakini pia.”amesema Justine.
Amesema kuwa kufuatia mkasa huo wa mkanganyiko alienda polisi kutoa taarifa na hospitali ya rufaa ambako alielezwa alipewa majibu ya kuwa watabadilisha vibali vya ruhusu vya kuchukua miili kama hakuna malalamiko kutoka pande zote mbili.
Justine amesema alikwenda pia chumba cha kuhifadhia maiti kujiridhisha kwa kuangalia mwili wa, Gervas Chondomba na kutambua kuwa ndio yeye na mwili wa Mark Mkude aliyezikwa katika makaburi ya Bigwa Mbuyuni umerudishwa katika chumba hicho ili ndugu zake kuendelea na taratibu za mazishi.
Mkazi wa mtaa huo, Hamis Ibrahim amesema ameshiriki kufukua kaburi na wenzake watatu baada ya vijana wenzao kujiweka pembeni.
“Ni tukio la kustajabisha lakini tayari limetokea nimeweza kushiriki kufukua kaburi na kutoa jeneza lenye mwili wa Mark Mkude ambapo kaburi hilo limetumika kuzikwa, Gervas Mkoba Chondomba leo saa 7 mchana ambaye haswa alikusudiwa kuzikwa hapo badala ya aliyezikwa.”amesema Ibrahim.
Ibrahi amesema kazi ya kufukua kaburi ilianza saa 3 asubuhi na saa 4 asubuhi hiyo tayari jeneza lenye mwili wa Mark Mkude walikuwa wamelifikia na waliacha kulitoa ndani ya kaburi mpaka taratibu za kisheria zilipokamilika na kuutoa mwili huo kaburini saa 11 asubuhi leo na kupelekwa chumba cha kuifadhi maiti cha mkoa na ndugu kukabidhiwa mwili huo.
Mohamed Mkwama ambaye ni kaka wa marehemu amesema yametokea makosa madogo ya kukosa umakini wakati ndugu walipoenda kuutambua mwili wa marehemu jana kabla ya kurejea nao nyumbani kwa ajili ya shughuli ya mazishi.
“Hili limetokea kwa sababu ya kukosa umakini ndio maana limetokea lakini hawa wazee wote ni ndugu na wanatumia ubini wa Mkude nafikiri kwenye kutaja jina la Mkude ndiko kulikochanganya.”amesema Mohamed.
Mohamed amesema wazee hao wamefanana sura na majina ya ukoo walikuwa wakitumia “Mkude Mkoba” na licha ya kutokea hilo sasa Chondoma amezikwa saa 7 mchana makaburi ya Bigwa Mbuyuni huku Mark Mkude akizikwa makaburi ya Damu ya Yesu Bigwa Kola B kata ya Kilakala.
Social Plugin