Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amefanya mazungumzo kwa njia ya mtandao na Bi. Joy Phumaphi Katibu Mtendaji wa Taasisi ya ‘African Leaders Malaria Alliance’ (ALMA) pamoja na Bw. Li Chinbiao Mkurugenzi Mtendaji wa ‘Yorkool International Company’ kujadili fursa ya uwekezaji wa kiwanda cha kuzalisha vyandarua vya kisasa vyenye dawa 2 za kudhibiti mbu sugu wanaoeneza ugonjwa wa malaria.
Mazungumo hayo yanafanyika kufuatia kikao baina ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Bi. Joy Phumaphi Mwezi Novemba 2021 ambapo Rais Samia Suluhu Hassan aliitaka Taasisi hiyo kushirikiana na Wizara ya Afya nchini kutafuta wawekezaji ambao wataweka kuwekeza hapa nchini viwanda vya kutengeneza vyandarua vya kisasa vyenye dawa 2 za kudhibiti mbu wanaoambukiza ugonjwa wa malaria pamoja na kutoa utaalam kwa Watanzania hapa nchini.
Katika mazungumzo hayo Dkt. Mollel amesema Serikali inataka kutokomeza ugonjwa wa Malaria kabla ya mwaka 2030 na kusema kuwa uwekezaji wa viwanda vya vyandarua vyenye kudhibiti Malaria pamoja na taaluma utasaidia kutokomeza ugonjwa huo hapa nchini na kwa ukanda wote wa nchi za Afrika Mashariki.
Kwa upande wao Kampuni ya ‘Yorkool International’ wameonyesha nia ya kuja kuwekeza hapa nchini na kusema kuwa wapo tayari kushirikiana na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuwekeza kiwanda cha kutengeza vyandarua.
Dkt. Mollel ameagiza kuundwa kwa timu ya wataalam kwa kushirikiana na ALMA kuandaa mpango mkakati wa utekelezaji wa shughuli hiyo na kutoa mrejesho kwa viongozi wa Wizara.
Social Plugin