Ndege ya Shirika la AirAsia iliyokuwa ikisafiri kutoka Kuala Lumpur kuelekea katika Mji wa Tawai nchini Malaysia, imelazimika kutua kwa dharura baada ya nyoka kuonekana ndani ya ndege hiyo.
Katika tukio hilo ambalo ni nadra kutokea, nyoka huyo alionwa na abiria akiwa anatambaa ndani ya plastiki angavu ndani ya ndege ambapo rubani alipopata taarifa, alilazimika kukatisha safari na kutua kwa dharura katika Uwanja wa Ndege wa Kuching nchini humo.
Baada ya ndege kutua, wafanyakazi wa uwanja huo walipulizia dawa maalum ndani ya ndege na hatimaye wakafanikiwa kumtoa kisha safari ikaendelea.
Shirika la Habari la CNN, limemnukuu mkuu wa kitengo cha usalama kwa abiria wa shirika hilo la ndege, Liong Tien Ling akieleza kuwa matukio ya aina hiyo hutokea kwa nadra na walilazimika kutua kwa dharura kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa abiria waliokuwa ndani ya ndege.
Tukio kama hilo limewahi kutokea mwaka 2012 katika ndege ya Shirika la EgyptAir ambapo abiria mmoja alikuwa akimsafirisha nyoka aina ya Cobra kimagendo ambapo kwa bahati mbaya, nyoka huyo alitoka kwenye begi na kumgonga mmiliki wake mkononi na kusababisha taharuki kubwa ndani ya ndege.