RAIS MWINYI AIPONGEZA BENKI YA CRDB UZINDUZI WA MIKOPO ISIYO NA RIBA KWA WAJASIRIAMLI ZANZIBAR, BILIONI 60 ZATENGWA


Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametoa pongezi na shukrani kwa Benki ya kwa kukubali kushirikiana na Serikali yake katika kuwawezesha wajasiriamali na kuendeleza uchumi wa visiwa hivyo.


Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo katika uzinduzi wa Mikopo isiyo na riba kwa Wajasiriamali iliyopewa jina la “INUKA NA UCHUMI WA BULUU” ikiwa ni ushirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya CRDB, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idris Abdulwakil, Kikwajuni Zanzibar.
Katika hotuba yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa mikopo hiyo itakuwa kichocheo kikubwa kwa ukuaji wa uchumi wa Zanzibar. Amewataka wajasiriamali katika visiwa vya Unguja na Pemba kuchangamkia fursa hiyo ya kipekee kukuza mitaji na kuboresha biashara zao.

Alisema kuwa juhudi zinazofanywa na Benki ya CRDB katika kujenga uchumi wa Zanzibar ni nyingi na anaamini kwamba sasa zinafahamika vizuri na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano unaohitajika na kudumisha uhusiano mwema uliopo kwa faida ya pande zote mbili pamoja na wananchi wote kwa jumla.

“Benki ya CRDB leo mmedhihirsha uzalendo wa kweli kwa kuandika historia ya kuwa Benki ya kwanza nchini kutoa mikopo bila riba kwa wajasiriamali. Hii inaonyesha dhamira ya kweli mliyonayo katika kuboresha maisha ya wajasiriamali hapa Zanzibar,” amesema Rais Mwinyi.
Rais Dkt. Mwinyi alisema kuwa imani yake ni kwamba wajasiriamali wote watatoa ushirikiano mzuri kwa Benki ya CRDB na watachangamkia ipasavyo fursa zilizopo kwa kuzingatia taratibu zinazoongoza na kusimamia mikopo hiyo. Aliongeza kuwa vile vile wana uwezo na taaluma ya ujasiriamali, waadilifu na wana dhamira ya dhati ya kurejesha fedha hizo.

Alieleza kwamba mikakati ya Serikali ya kuwawezesha Wajasiriamali aliyoahidi sasa inatimia ikiwa ni pamoja na utoaji wa vitambulisho, ujenzi wa masoko, utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu, elimu, zana, mitaji, maeneo bora ya kufanyia kazi pamoja na utaratibu mzuri wa ulipaji kodi.

Aliwaahidi wajasiriamali kwamba Serikali itaendelea na juhudi za kuwapatia mitaji, masoko, elimu pamoja na kuweka mazingira rafiki ili waweze kuendesha shughuli zao kwa ufanisi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema Benki hiyo inalichukulia kundi la wajasiriamali kama kundi la kimkakati katika maendeleo ya Taifa kutokana na kujumuisha asilimia kubwa ya wananchi.

Nsekela alisema kuwa kupitia program hiyo ya “INUKA NA UCHUMI WA BULUU” kimetengwa kiasi cha shilingi bilioni 60 kwa ajili ya wajasiriamali visiwani humo huku akisisitiza kuwa mikopo itatolewa bila riba kama walivyokubaliana na Serikali. Alibainisha kuwa mbali na uwezeshaji huo wa kifedha, programu hiyo pia itahusisha mafunzo ya ujasiriamali ambayo yanaendeshwa katika mikoa yote Zanzibar.

“Mheshimwa Rais utaratibu wa mikopo hii ni rahisi sana na tutakuwa tukiitoa kwa kushirikiana na Serikali katika hatua zote za utambuzi na upitishwaji wa mikopo ili kuhakikisha makundi yote stahiki ya wajasiriamali yananufaika,” amesema Nsekela.
Akielezea utaratibu wa utoaji mikopo hiyo kupitia programu ya “INUKA”, Nsekela amebainisha kuwa benki hiyo imezingatia mazingira ya soko la Zanzibar na kuwa mikopo itatolewa kupitia mfumo wake wa kutoa huduma unaozingatia misingi ya dini ya kiislamu “CRDB Al Barakah Banking”, pamoja na mfumo wa kawaida kwa wale watakaohitaji.

Shughuli zilizopewa kipaumbele katika program hii ya “INUKA” ni zile ambazo zimeanishwa katika sera ya Uchumi wa Buluu ikiwamo; uvuvi, ufugaji wa samaki, pamoja na kilimo cha mwani. Kwa kutambua changamoto zilizozikumba biashara nyingi kutokana na janga la COVID19, Benki pia imeainisha maeneo mengine ya kimkakati ya biashara ambayo yanahitaji kuongezewa nguvu ya uwezeshaji. Takribani watu laki saba wanatarajiwa kunufaika na fedha hizo, huku zaidi ya ajira laki moja zikitarajiwa kuzalishwa.
Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi akipokea maelezo kwa mmoja wa wajasiriamali waliohidhuria hafla ya uzinduzi wa ushirikiano baina ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Benki ya CRDB kupitia Mikopo ya Wajasiriamali ya INUKA NA UCHUMI WA BULUU. Katika makubaliano hayo Benki ya CRDB itakuwa ikitoa mikopo bila riba, pmaoja na mafunzo ya uendeshaji bora wa biashara kwa wajasiriamali Zanzibar. Kushoto kwake ni, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omari Said Shaaban, na kulia kwake ni, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post