Wafanyakazi wa Mamlaka ya usimamizi wa bima wakiwa na viongozi katika mafunzo ya elimu ya bima kwa waandishi wa habari yaliyofanyika leo katika ukumbi wa Nyanza uliopo Jijini Mwanza
Waandishi wa habari wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi kutoka Mamlaka ya usimamizi wa bima (TIRA) katika mafunzo ya elimu ya bima yaliyofanyika Jijini Mwanza
Naibu Kamishna wa Mamlaka ya bima Taifa, Khadija Said akifungua mafunzo ya elimu ya bima kwa waandishi wa habari leo Jijini Mwanza
Meneja wa Mamlaka ya usimamizi wa bima (TIRA) kanda ya ziwa, Sharif Hamadi akizungumza kwenye mafunzo ya kuwajengea uelewa wa bima waandishi wa habari yaliyofanyika leo Mkoani Mwanza
***
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mamlaka ya usimamizi wa bima Tanzania (TIRA) imetoa elimu ya bima kwa wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari Mkoani Mwanza.
Elimu hiyo ya bima imetolewa leo Alhamisi Februari 24,2022 katika ukumbi wa Nyanza uliopo Jijini Mwanza.
Akizungumza katika mafunzo hayo Meneja wa Mamlaka ya usimamizi wa bima (TIRA) Kanda ya ziwa, Sharif Hamadi amesema kuwa lengo la kutoa elimu ya bima kwa waandishi wa habari ni kuwajengea uelewa ili iwe rahisi kwao kuweza kufikisha elimu hiyo kwa Jamii.
Amesema kuwa waandishi wa habari ni muhimili mkubwa sana wakuweza kuhabarisha Jamii juu ya ukataji wa bima mbalimbali hali itakayosaidia kuepukana na majanga.
" Wenye bima za afya wanapougua wanakuwa na uhakika wa kutibiwa ila kwa wale ambao hawana bima inakuwa ni shida sana ukizingatia ugonjwa unakuja bila hodi na unaweza ukakukuta huna hela, sanjari na unapokuwa umeikatia nyumba yako bima hata ikitokea ikaungua bima inakulipa fidia na ndio maana halisi ya bima kulipa fidia pale majanga yanapo kukuta", amesema Hamadi
Amewasisitiza waandishi wa habari kwenda kuwa chachu katika Jamii kwakutoa elimu na kuwashawishi Wananchi kukata bima ya afya, mazao, nyumba, Magari, ili waweze kupata fidia pindi majanga yanapowakumba.
Awali akifungua mafunzo hayo Naibu Kamishina wa Mamlaka ya bima Taifa, Khadija Said amesema kuwa waandishi wa habari watumie kalamu zao kuielimisha Jamii ili waone umuhimu wa bima kuanzia ngazi ya familia hadi Taifa kwaujumla.
Amesema kuwa Jamii inapaswa itambue kuwa Baba au Mama anapo kuwa na bima ya maisha hata kama janga la kifo litatokea famila husika itaendelea kustawi kwani Watoto wataenda shule, huduma mbalimbali zitaendelea kupatikana tofauti na familia isiyokuwa na bima.
"Biashara yenye kinga ya bima ni biashara endelevu,pia bima ni mlinzi wa uchumi wetu, tukilinda uchumumi wa familia zetu tumelinda uchumi wa Taifa na hivyo kuendelea kukua kiuchumi", amesema Said.
Rose jacobo ni miongoni mwa waandishi wa habari alieshiriki mafunzo hayo amesema kuwa kutokana na elimu aliyoipata atakuwa balozi mzuri wa kuandika habari za bima sanjari na kutoa elimu kwa jamii inayomzunguka ili waweze kufahamu umuhimu wa kukata bima zitakazo wasaidia pindi majanga yanapo wakumba.