Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAWATUNUKU VYETI WAWINDAJI MAHIRI WALIOKIDHI VIGEZO

 Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.Damas Ndumbaro akiongea wakati wa hafla ya kuwatunuku vyeti kampuni nne za uwindaji na Utalii Jijini Dodoma

*****
Na Dotto Kwilasa, Malunde 1 Blog-DODOMA.

WIZARA ya Maliasili na Utalii kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania(TAWA) imekabidhi vyeti kwa wawekezaji waliokidhi vigezo na  kufanikiwa kupata maeneo ya uwekezaji mahiri katika maeneo yaliyoainishwa kwa uwindaji na Utalii (SWICA).

Kampuni zilizotunukiwa vyeti ni nne ambazo ni Green Nile Safari  LTD,Grumet  Services Ltd,Mwiba Holding LTD,na kampuni ya ndani ya Mkwawa Hunting Safari zote zikiwa zinasimamiwa na(TAWA).

Akiongea katika hafla ya kutunuku vyeti Kampuni hizo Jijini Dodoma ,Waziri mwenye dhamana ya Utalii Dkt. Damas Ndumbaro amesema serikali itaendelea kutoa fursa kwa wawekezaji kwenye sekta ya utalii na kuendelea kuboresha huduma za kitalii nchini ikiwemo kurahisisha  upatikanaji wa leseni za shughuli za utalii pamoja na miundombinu ya malazi.

Pia Waziri Ndumbaro ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wawekezaji wa kigeni kuwekeza nchini huku akiitaja Tanzania kuwa ni salama, yenye amani na demokrasia na kwamba Wizara anayoiongoza imefungua milango kwa wawekezaji wote kuja kuwekeza nchini.

"Sisi kama Wizara ya Maliasili na Utalii, falsafa yetu ni moja tu, mteja ni mfalme, niwahakikishie kuwa tuko tayari kukutana na mwekezaji wa aina yoyote ile na muda wowote ili kujadili changamoto zitakazojitokeza,"amesema Dkt. Ndumbaro.

Aidha amewataka wawekezaji  wazawa pamoja na wa kigeni kuchangamkia fursa za uwekezaji wa uwindani na utalii ili kuimarisha maliasili na kukuza pato ghafi la uchumi wanchi.

Kuhusu suala la uvamizi wa maeneo ya uhifadhi kutokana na shughuli za binadamu Dkt.Ndumbaro ameitaka TAWA kuendelea kujiimarisha zaidi  hali itakayosaidia kuendelea kulinda na kuhifadhi maeneo muhimu ya uhifadhi.
 
"Katika hili lazima niwapongeze TAWA,licha ya kwamba ni Mamlaka changa lakini inafanya vizuri,endeleeni  kuelekeza nguvu ya usimamizi wa uhifadhi wa wanyamapori nchini,ondoeni uvamizi wa aina yoyote,hii itasaidia kuitangaza vizuri nchi yetu kwani bado tunahitaji kujitangaza zaidi "amesema.
         
Naye Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi wa TAWA,Meja Jenerali  Mstaafu Hamis Semfuko amesema Matarajio ni ukusanyaji wa zaidi ya Bilioni 23 za kitanzania kwa mwaka kutokana na uwekezaji wa kampuni hizo nne zilizojikita kwenye nyanja ya uwindaji na utalii.

Amesema Hali hiyo itahamasisha na kuwavutia Wazawa kushiriki zaidi katika kuwekeza kwenye utalii na kwamba bodi hiyo itaendelea kusimamia vyema katika kuhakikisha mapato yatokanayo na wanyamapori yanawanuwaisha watanzania.

"Miradi hii inaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye maeneo ya SWICA,niwahakikishie TAWA imeweka mipango madhuhuti, kuhakikisha miradi yote ambayo imekusudiwa kutekelezwa kwa kutumia fedha zetu , ndani ya muda uliopangwa na kwa ubora uliokusudiwa,"amesisitiza Mwenyekiti huyo wa bodi ya TAWA.

Kwa upande wa wawekezaji hao wamesema,kufuatia kuaminika kiasi cha kutunukiwa vyeti hivyo watajitahidi kuongeza bidii zaidi katika kujiimarisha kwenye uwindaji na na Utalii unao hifadhi mazingira na kulinda wanyamapori.

 Akizungumza mara baada ya kutunukiwa Cheti mwakilishi kampuni ya GREEN  NILE SAFARI’S LTD   Selem  Baileith amesema wataendelea kulinda uhifadhi na kwamba shughuli zao zote zitazingatia kanuni na utaratibu wa uhifadhi.

Naye mwakilishi wa kampuni ya Mkwawa Hunting  Safari  Benson  Kibonde, ameishukuru Serikali kwa juhudi inazofanya kuhakikisha shughuli za Uhifadhi zinapata mwelekeo kama wananchi wanavyotazamia.

"Tunaishukuru sana Serikali,sisi kama wazawa,tutatumia akili na nguvu zetu zote  katika masuala mazima ya uwekezaji katika tasnia ya Utalii na  Uhifadhi wa Wanyamapori, ili kuongeza  ukuaji wa sekta ya utalii nchini,"ameeleza

Utaratibu wa kuwapata wawekezaji kwa njia ya umahiri wa maeneo maalum yaliyoainishwa kwa uwindaji  umefanyika kwa mujibu wa kanuni za SWICA mwaka  2020   ambazo zimempa mamlaka  kamishna wa uhifadhi,TAWA ,kuunda  timu ya majadiliano na  kubaini kuwa  mpango huu una tija  katika kuongeza mapato yatokanayo na shughuli za utalii na  kuruhusu uwekezaji wa miaka 30.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com