Watu kadhaa wakiwemo wafanyakazi 12 wa kampuni ya Azam Media wamejeruhiwa baada ya gari la kampuni hilo walilokuwa wakisafiria kutokea mkoani Mbeya kuelekea jijini Dar es Salaam, lenye namba za usajili T735DHQ aina ya Toyota Hiace kugongwa na lori lililopata hitilafu katika mfumo wa breki, tukio lililotokea leo Februari 13, 2022 katika eneo la Kitonga mkoani Iringa.
Taarifa iliyotolewa na Kampuni ya Azam Media, imeeleza kwamba wafanyakazi wake hao, walikuwa wakitokea mkoani Mbeya walikoenda kwa ajili ya kurusha matangazo ya moja kwa moja ya Ligi Kuu ya NBC na kwamba, wamesaidiwa na Jeshi la Polisi na wasamaria wema na kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa kwa matibabu zaidi.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa ajali hiyo, lori hilo lilipata hitilafu katika mfumo wa breki na kuanza kurudi nyuma kwa kasi na ndipo lilipoligonga gari hilo la Azam lililokuwa nyuma yake.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Allan Bukumbi amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kueleza kuwa jeshi la polisi lipo eneo la tukio kwa ajili ya kuwasaidia wote waliopata majeraha na kueleza kwamba taarifa kamili itatolewa baadaye.
Social Plugin