Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATATU WAKAMATWA WAKIUZA PEMBEJEO ZA SERIKALI

Viuatilifu vya zao la pamba 

Na COSTANTINE MATHIAS, Maswa.

WAFANYABIASHARA watatu wilayani Maswa mkoani Simiyu wamekamatwa kwa kosa la kujihusisha na uuzaji wa viuatilifu vya zao la pamba vilivyotolewa na serikali kwa ajili ya wakulima wa pamba.

Akizungumza jana na waandishi wa Habari, Afisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa halmashauri ya wilayani humo, Robert Urasa alisema kukamatwa kwa wafanyabiashara hao kunatokana na msako kwa wanaouza pembejeo kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo mnadani.

Aliwataja wafanyabiashara hao kuwa ni Samson Sikambundwa, Paschal Siwingwa na Mashaka Daudi wakazi wa Maswa na wamekamatwa na Maafisa wa kilimo wakiuza dawa za kuulia wadudu kwenye zao la pamba zilizotolewa na serikali kupitia bodi ya pamba nchini kinyume cha sheria na taratibu.

Alisema wamekuwa wakipokea malalamiko mengi ya kuwepo kwa viuawadudu vilivyotolewa na serikali ikiwa ni mkopo kwa wakulima wa pamba, lakini vimekuwa vikiuzwa kwenye maeneo ya minada kutoka kwa wakulima na viongozi wasio waaminifu.

‘’Tumeamua kufanya msako kwa watu wote kwenye maduka yanayouza pembejeo pamoja na minadani…kuna baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu walipatiwa viuadudu ili vitumike kunyunyuzia mashamba katika musimu wa kilimo 2021/22, lakini wanaviuza tutawakamata wote’’, alionya Urasa.

Alisema kuwa kitendo kilichofanywa na wafanyabiashara hao ni Uhujumu Uchumi na watahakikisha mtandao mzima walioshirikiana kuhujumu viuadudu hivyo wanakatwa na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Urasa alisema baada ya kupata taarifa kuwepo kwa viuadudu hivyo katika mnada wa Maswa Mjini walifanya upekuzi kwenye maeneo ya wafanyabiashara hao na kukamata Hekapaki 230 zenye thamani ya shilingi 917,800/= zilizokuwa na nembo ya Bodi ya Pamba Tanzania(TCB) zikiuzwa kinyume na utaratibu.

Alitaja thamani ya viuadudu vilivyokamatwa kwa kila mfanyabiashara kwenye mabano, Samson Sikambundwa (Sh 132,000), Paschal Siwingwa (Sh 49,000) na Mashaka Daud (Sh 736,800).

Alisema wafanyabiashara hao wamefikishwa kituo cha Polisi wilaya ya Maswa na wanatarajiwa kufikishwa Mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili mara baada taratibu za jeshi la polisi kukamilika.

Aliongeza kuwa zoezi hilo ni endelevu na hawatovumilia kuona upotevu wa fedha za serikali pia waliwataka wafanyabiashara wote kuacha tabia hiyo vinginevyo hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayebainika kuhusika na biashara hiyo Haramu.

Naye Mkaguzi wa Bodi ya Pamba, Ally Mabrouck alisema amesikitishwa na kitendo cha baadhi ya wakulima waliopewa viuadudu hivyo na viongozi waliopewa jukumu la kugawa viuadudu kuviuza kwa wafanyabiashara wakati vimetolewa na serikali kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

Alisema kwa kiasi hicho cha viuadudu kilichokamatwa  kitasababisha hekta 230 za zao la pamba kutonyunyiziwa dawa na hivyo kusababisha wilaya hiyo kutofikia malengo yake ya kuzalisha pamba tani 130,000 kama ilivyotarajia.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge baada ya kupokea taarifa hiyo alisema ameona pembejeo zilizokamatwa ambazo ni ruzuku ya serikali zinazotakiwa kwenda kwa wakulima moja kwa moja.

"Kuna kodi ya wananchi ilipelekwa wilayani humo ili kuinua sekta ya kilimo ya zao la pamba, lakini baadhi ya watu wasio na uzalendo wameamua kuzifanyia biashara pembejeo hizo hivyo ni lazima hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa watu wote watakaobainika kuhujumu viuadudu hivyo’’ ,alisema Kaminyoge.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com