Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora limekamata mtandao wa watu 9 ambao wametajwa kuhusika na tuhuma za mauaji pamoja na kuendesha biashara ya mauziano ya viungo mbalimbali vya sehemu ya mwili wa binadamu.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora, ACP Richard Abwao amesema mtandao huo umekamatwa ikiwa ni siku chache tu baada ya kutokea mauaji ya kinyama ya binti mmoja huko wilayani Sikonge Mkoani Tabora.
Amesema kufuatia tukio la mauji hayo watu watatu walikamatwa baada ya kutiliwa mashaka ambapo walimtaja mganga wa kienyeji ambaye amekuwa akinunua viungo vya mwili ikiwemo sehemu za siri za jinsia zote pamoja na matiti.
Aidha, mganga huyo ambaye hakutajwa jina lake kutokana na sababu za kiuchunguzi alikiri kuhusika na tuhuma hizo huku naye akimtaja mtu ambaye amekuwa akimuuzia viungo hivyo vya mwili ambaye pia alihojiwa na kukubali kufanya hivyo pamoja na kutekeleza matukio mengine ya mauaji ya kinyama yaliyo ambatana na kukinga damu katika chupa ambayo amekuwa akiiuza kwa kiasi cha shilingi laki 6.