****************
Na John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa na Balozi wa China nchini Tanzania. Mhe, Chen Mingjian wameshiriki kwenye hafla ya Uzinduzi wa Mashindano ya Olympic ya michezo ya majira ya baridi yanayozinduliwa rasmi leo Februari 4, 2022 jijini Beijing kwa kucheza mchezo wa mpira wa meza kwenye Ubalozi wa China nchini Tanzania.
Mashindano ya mwaka huu yatafanyika katika miji ya Yanqing na Chongli nchini China.
Katika hafla hiyo Mhe. Waziri Mchengerwa na Katibu Mkuu wake Dkt. Hassan Abbasi walikabidhiwa zawadi na Mhe. Balozi.
Mhe. Mchengerwa amesema Tanzania imekuwa na uhusiano mzuri na wa muda mrefu kwenye Sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo ulioasisiwa viongozi wa mataifa hayo mawili ambao hauna budi kuendelezwa na kurithishwa vizazi hadi vizazi.
Aidha, amesema Rais wa Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan ana matarajio makubwa ya mahusiano wa nchi hizi mbili.
Ametumia tukio hilo kuiomba nchi ya China kusaidia kukuza na kuendeleza lugha ya Kiswahili duniani.
"Ni mategemeo yetu kuwa mtawachukua wataalam wetu wa kiswahili ili wakafundishe katika vyuo vyenu vikuu" amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Pia katika hafla hiyo Mhe. Balozi na Mhe. Waziri wamekubaliana Wizara kuandaa andiko la mashirikiano ( MoU) katika Sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo ili kuziendeleza sekta hizo.
Pia ameiomba Serikali ya China kusaidia mkakati wa Serikali wa kuuimarisha miundombinu ya michezo hususan viwanja vya michezo ili Tanzania pia ipige hatua kwenye michezo.
Pia, ameiagiza Kamati ya Olympic nchini kujipanga na kuandaa wachezaji ambao mwakani watakwenda kushindana, siyo kutalii.
Amepongeza Nchi ya China kwa kuanza mwaka mpya na kumpongeza Balozi kwa kuteuliwa kuiwakilisha nchi yake hapa Tanzania.
Kwa upande wake Mhe. Balozi amesema nchi yake inaitazama Tanzania kama rafiki wa kwanza katika Bara la Afrika na kwamba imekuwa na mabadilishano ya watu kuja kujifunza na mafunzo mbalimbali kabla ya corona.
Hafla ya leo imeshirikisha Balozi wa Tanzania nchini China Mbelwa Kairuki, viongozi wa Kamati ya Olympic, wadau mbalimbali wa Michezo na kupambwa na wasanii watatu walioshinda kwenye tamasha la BSS la mwaka huu.