Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda akiongea mara baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye ujenzi wa Ofisi za TAEC Kikombo jijini Dodoma.
Mkurungenzi Mkuu wa TAEC, Profesa Lazaro Busagala akifafanua jambo wakati wa uwekaji jiwe la msingi ambapo ameeleza kuwa Serikali kupitia tume hiyo imeweka mikakati ya kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kujenga Ofisi hiyo ambayo itakuwa na maabara tano za sampuli za vyakula, mazingira,tathimini ya viwango vya mionzi kwa wafanyakazi na kuwaepusha na madhara,maabara ya matengenezo ya vifaa vya nyuklia ,maabara ya sampul za mazingira,maabara ya ulinzi na usalama wa kinyukilia .
***
Na Dotto Kwilasa-Malunde 1 Blog-DODOMA.
WAZIRI wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda ameweka jiwe la msingi la maabara na Ofisi ya Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC)Kikombo jijini Dodoma huku akiitaka tume hiyo kuwajengea uwezo na kuwapa hamasa wanafunzi wa kitanzania kusomea masomo ya sayansi ili kuwa na wanasayansi wengi kwa uchumi wa nchi.
Akiongea mara baada ya kuweka jiwe la msingi jana,Prof.Mkenda amesema kuwepo kwa Ofisi hizo Jijini Dodoma kutatoa fursa kwa wanafunzi mbalimbali kufika ili kujifunza jinsi ambavyo wanaweza kupata manufaa ya uwepo wa tume hiyo na kujifunza kwa vitendo wanayosoma darasani.
Amesema,hatua hiyo itaongeza juhudi za kuwaandaa Wanasayansi wa kutosha na kwamba ipo haja ya wizara hiyo kuhakikisha vijana waliofanya vizuri kwenye masomo ya Sayansi wanapata ufadhili wa kusoma Vyuo vikuu nje ya Nchi.
Ameeleza mkakati wa Serikali kuwa ni kuhakikisha vijana waliofanya vizuri kwenye masomo ya Sayansi wanapata ufadhili (schoolaship) kwenye masomo yao ili wawe wajuzi na wabobezi.
"Kwa sasa tumepiga hatua kubwa ,ujenzi huu ukikamilika utakuwa na manufaa kwa jamii mzima,Kwa wanafunzi baadhi ya mashine walikuwa wanazisoma darasani tu, lakini jambo la kufurahisha wataziona kwa macho yao na kuonyeshwa kwa vitendo na jinsi zinavyoweza kufanya kazi na kuleta tija kwa Taifa ,
Tunahitaji Wanasayansi tuna jukumu la kusomesha Watanzania masuala ya nguvu za Atomiki hivyo nawaomba TAEC kutenga fedha ili Wanafunzi bora Kabisa wa sayansi wapate ufadhili,tukitenga fedha kila mwaka watakuwa wakienda kusoma nchi nyingi zilizoendelea kisayansi,"amefafanua.
Amesema nchi inahitaji vijana wabobezi wa Sayansi na Teknolojia ili watumike kukuza uchumi na kwamba kwa kutambua umuhimu huo kuna mkakati wa kukutana na Watanzania wanaofundisha Vyuo vikuu vya nje ili wafungue milango na kuona ni kwa jinsi gani vijana wa Tanzania watapata ufadhili.
"Tunao watanzania wengi wanaofundisha Vyuo vikuu nje ya Nchi, tutakaa nao ,watatufungulia milango kuona namna gani tutawezesha vijana wetu,pia tuna mkakati mwingine wa kuongea na balozi mbalimbali kuhusu vijana wanaofaulu vizuri masomo ya Sayansi wapate ufadhili ambapo pia Serikali nayo itakuwa na mchango wake katika kufanikisha jambo hilo,"amesema Waziri Mkenda.
Aidha, Waziri Mkenda ameipongeza TAEC kwa kuwa na maarifa ya kuwezesha kupima kiwango cha mionzi katika vyakula kutoka nje ya nchi Kwa kushirikiana vyema na taasisi mbalimbali za Serikali hususani Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TMDA) kujua kama muhusika ana kibali na kuhakikisha kwamba watanzania na wananchi hawapati madhara.
Kutokana na hayo Mwenyekiti wa Bodi ya TAEC, Profesa Joseph Msambichaka amesema wanatazamia kuanzisha ufadhili (schoolaship) kwa wanafunzi waliofanya vizuri masomo ya Sayansi kwenda kusomea Teknolojia ya nyuklia kwa matumizi salama ya mionzi na kuendeleza teknolojia ya nyukilia .
"Tunategemea kuanzisha mafunzo katika Sayansi ya nyuklia kwa kutumia wataalam waliopo ATEC,tunaomba pia kuangaliwa kwa suala la kuondoa tozo ambazo si za lazima katika mionzi,"amesema.
"TAEC inajivunia kwa uwezo wanaojengewa na Serikali ambao umeifanya kuwa ni tume pekee kwa upande wa Afrika ya Mashariki na kati yenye mitambo ya kisasa ambayo husaidia sana wananchi kuwa salama na ukizingatia kwamba shughuli nyingi za Serikali hutegemea mionzi hiyo ya asili na ya kutengeneza,"amesema.
Naye Mkurungenzi Mkuu wa TAEC, Profesa Lazaro Busagala amesema Serikali kupitia TAEC imeweka mikakati ya kusogeza huduma karibu na wananchi Kwa kujenga Ofisi hiyo ambayo itakuwa na maabara tano za sampuli za vyakula, mazingira,tathimini ya viwango vya mionzi kwa wafanyakazi na kuwaepusha na madhara,maabara ya matengenezo ya vifaa vya nyuklia ,maabara ya sampul za mazingira,maabara ya ulinzi na usalama wa kinyukilia .
Amesema ujenzi huo Wenye eneo la mita za mraba 1602 hadi kukamilika kwake utagharimu Shilingi bilioni 3.8 gharama hizo ni pamoja na kuweka mandhari nzuri na uzio.
"Jengo hili litakuwa na Ofisi 27 kwa kuhusisha chumba cha mkutano pamoja na sehemu maalumu ya kufanya mazoezi Kwa wafanyakazi ilikuwasaidia kujenga afya,lengo ni kuhakikisha kwamba wafanyakazi wetu wanaofanya kazi katika sekta hii hawadhuriki,"amesema