Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amefanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Taasisi ya Ushirikiano wa Kimataifa wa Masuala ya Kibinadamu kutoka nchini Urusi Bw. Yevgeny Primakov leo tarehe 03 Februari 2022 katika ofisi za Wizara jijini Dodoma.
Bw. Primakov ameambatana na Balozi wa Urusi nchini, Mhe. Yuri Popov pamoja na Mjumbe kutoka Serikali ya Urusi, Bw. Egor Utkin.
Wawakilishi hao kutoka Serikali ya Shirikisho la Urusi waliwasilisha ujumbe wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kutoka kwa Rais wa Shirikisho la Urusi Mhe. Vladimirovich Putin.
Pamoja na mambo mengine viongozi hao walijadili juu ya kuimarisha ushirikiano uliopo na kwamba kwa sasa Tanzania na Urusi zinajikita zaidi katika kufungua maeneo mapya ya ushirikiano katika sekta za biashara, uwekezaji, utalii na masuala mengine ya kiuchumi kwa maslahi mapana ya mataifa hayo.
Waziri Mulamula alieleza kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano mzuri na wa kihistoria ambao uliasisiwa na Waasisi wa Mataifa hayo mawili.