Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akiendesha Basi dogo aina ya TATA la kikundi cha Vijana na Mapambano
Na Marco Maduhu, Shinyanga.
MKUU wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, amekabidhi Basi dogo aina ya TATA kwa kikundi cha vijana na mapambano Manispaa ya Shinyanga, ambalo litakuwa likitumika kubeba wanafunzi kwa ajili ya kuwapeleka shule, na baadaye kubeba abiria na saa 10 alasiri kuwarudia wanafunzi majumbani hadi saa 12 jioni, kisha kuendelea na ubebaji wa abiria.
Makabidhiano hayo yamefanyika Ijumaa Machi 11,2022 katika eneo la Manispaa ya Shinyanga, na kushuhudiwa na Meya wa Manispaa ya Shinyanga Elias Masumbuko, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa Baraka Shemahonge, baadhi ya wananchi na watumishi wa Halmashauri hiyo ya Manispaa ya Shinyanga.
Akizungumza wakati wa kukabidhi basi hilo, Mboneko amewataka vijana hao walitunze pamoja pesa ambazo wanazipata wazifanyie maendeleo na ikiwezekana waongeze basi jingine na kuinuka kiuchumi.
“Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan alisema mikopo hii asilimia 10 ya Halmashauri ifanyiwe vitu vikubwa kwa kuonekana miradi yenye tija, na leo Manispaa ya Shinyanga tunakabidhi Basi katika kikundi cha vijana, pamoja na Mashine ya kutotoreshea vifaranga vya kuku kwa kikundi cha wanawake,”alisema Mboneko.
“Wanafunzi wetu walikuwa wakipata shida sana ya usafiri kwenda shule, na mimi nilipiga marufuku kupewa lifti bali wavulie sababu Serikali tutalifanyia ufumbuzi tatizo hilo, na leo tumekabidhi vijana Basi kwa ajili ya kuwapeleka shule na kuwarudisha,”aliongeza.
Aidha, alitoa onyo pia kwa wanafunzi wasije wakachorachora Basi hilo pamoja na kuharibu viti, bali wawe wastarabu ili waendele kunufaika na matunda ya Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, huku akiwasihi wasome kwa bidii na kusiwepo Ziro hata moja kwenye mitihani yao.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa wilaya, alitoa maekelezo ya Nauli kuwa Basi hilo litakuwa likibeba wanafunzi kwa Sh,200 na watu wazima Sh.500.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Jomaary Satura, alisema Manispaa hiyo ina mpango wa kutoa Mabasi mengine manne kwa ajili ya kazi hiyo ya kubeba wanafunzi na baadaye abiria wa kawaida.
Naye Afisa Maendeleo ya jamii Manispaa ya Shinyanga John Tesha, alisema kikundi kicho cha vijana walikikopesha Sh. milioni 60 kwa ajili ya kununua Basi hilo, ambapo kiasi kingine cha fedha walikiongeza wao wenyewe, huku akibainisha kuwa kwa upande wa mashine ya kisasa ya kutotoresha vifaranga vya kuku wameinunua kwa Sh. milioni 2.2.
Aidha alisema Halmashauri hiyo imeendelea kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu, kuwa kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Disemba (2021-2022) kuwa kimetolewa kiasi cha fedha Sh.milioni 175.0
Alifafanua kuwa fedha hizo za mkopo zimetolewa kwa mchanganuo ufuatao, ambapo vikundi vitano vya wanawake vimepatiawa Sh. milioni 46, Vijana vikundi Vinne Milioni 126, kikundi kimoja cha watu wenye ulemavu Sh.milioni 3.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kikundi cha Mapambano ambao wamekabidhiwa Basi hilo Jasamila Maduhu, ameipongeza Serikali kwa kuwapatia mkono huo wa Basi ambalo litabadili maisha ya kiuchumi na kubainisha kuwa wamelinunua kwa bei ya Sh, milioni 105.
Chanzo - Shinyanga Press Club blog
Social Plugin