Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi amewaonya watendaji wa Mamlaka ya Maji Vijini, (RUWASA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, akiwataka kuacha mara moja tabia ya kuchafuana kwa lengo la kusaka madaraka na badala yake wafanye kazi kwa pamoja kuhakikisha miradi ya maji inayotekelezwa na Serikali kwenye maeneo yao inakamilika kwa wakati na wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama.
Mhandisi Maryprisca Mahundi ametoa onyo hilo wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mkula wilayani Busega wakati akikagua mradi wa maji wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni mbili unaotekelezwa na Serikali kwa ajili ya kuhdumia wananchi wa vijiji vitano vya eneo hilo.
Amewataka watendaji hao kuanza kufanya kazi kwa pamoja ili kuleta tija na kudai kuwa tabia ya kuchafuana itasababisha halmashauri hiyo kuwapoteza viongozi wenye uwezo wa kuwasaidia wananchi kupata maji.