Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

LGTI KUUNGA MKONO JUHUDI ZA RAIS SAMIA KWA KUTOA HUDUMA BORA ZINAZOIMARISHA UTAWALA BORA


Mkuu wa chuo cha Serikali za mitaa Hombolo(LGTI)Dkt. Mpamila Madale akiongea na Waandishi wa habari kuhusu namna chuo hicho kinavyotekeleza ujenzi wa madarasa na nyumba za walimu ili kuunga mkono uhudi za Serikali katika kuchochea elimu nchini.
Naibu Mkuu wa LGTI Dkt. Michael Msendekwa akieleza namna chuo hicho kilivyojipanga kuendeleza elimu yenye viwango vya juu Kwa kuweka sawa mitaala itakayowezesha wanafunzi kumaliza masomo wakiwa na uwezo mzuri.
Chumba Cha darasa la kisasa katika chuo Cha Serikali za mitaa Hombolo kikiwa kimekarabatiwa hali itakayowezesha wanachuo kusoma kwa ari na kuwa na uwezo wa kuhitimu kwa ubora unaokidhi soko la ajira .

Na Dotto Kwilasa-Malunde 1 Blog-DODOMA

KATIKA kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Chuo cha Serikali za Mitaa Hombolo-Dodoma (LGTI) kimetumia zaidi ya shilingi bilioni 1.8 kujenga madarasa mapya,nyumba za watumishi, jengo la utawala na Campus ya Dodoma ili kuwezesha huduma bora zitakazo wajengea wananchi uwezo wa kuimarisha utawala bora.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Mpamila Madale wakati akiongea na Waandishi wa habari chuoni hapo kuhusu mafanikio yaliyopatikana LGTI ndani ya mwaka mmoja wa Rais Samia na kueleza lengo la kufanya hivyo ni kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya sita katika sekta ya elimu huku tukijipanga kutoa wahitimu ambao watakuwa na uwezo wa kujiajiri na kuajiriwa.

Amefafanua kuwa Shilingi milioni 550 ni kwa ajili ya kukarabati nyumba za wafanyakazi,mabweni na maktaba wakati Shilingi milioni 907 ni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la utawala kwa awamu ya kwanza ambalo litagharimu shilingi bilioni 4 hadi kukamilika kwake,Milioni 350 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, Shilingi milioni 255 kwa ujenzi wa Campus ya Dodoma mjini utakaogharimu shilingi bilioni 14 mpaka kukamilika kwake.

"Kwa kutambua umuhimu wa kuwafikia walengwa wa elimu,Serikali ya awamu ya sita imetupatia eneo lililokiwa Ofisi ya zamani ya mkuu wa Mkoa wa Dodoma Ili kujenga kampasi kubwa ya kisasa,LGTI tunamshukuru sana,na niseme wazi kuwa tuna imani naye na tutashirikiana naye bega kwa bega kufanikisha lengo la Serikali katika kutoa huduma bora, "amesisitiza.

Mkuu huyo wa LGTI ametaja pia mafanikio mengine ambayo yamepatikana katika kipindi cha awamu ya sita chuoni hapo kuwa ni pamoja na kutunza mazingira kwa kupanda miti zaidi ya 1000 hali inayo saidia kuweka mandhari safi na kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika masuala ya uhifadhi.

Kwa upande wake,Naibu Mkuu wa Chuo hicho,Taaluma,Utafiti na Ushauri,Dkt.Michael Msendekwa amesema wamejipanga kuendelea kutoa elimu yenye ubora ikiwa ni pamoja na kuiweka sawa mitaala ambayo itawafanya wanafunzi watoke wakiwa na uwezo wa kujiari na kuajiriwa.

Dkt. Msendekwa amesema wameongeza baadhi ya kozi pamoja na kuwapeleka wafanyakazi kwenda kusoma zaidi ili kuongeza ubora wa elimu katika chuo hicho.

"Chuo kimejipanga kukabiliana na changamoto ya ukatili wa kijinsia ambao umeendelea kujitokeza katika jamii kwa kuongeza baadhi ya kozi ambazo zitasaidia kulinda mmonyoko wa maadili,"amesema.

Naibu Mkuu wa Chuo hicho ,Mipango,Fedha na Utawala,Mashala Yusuph ameyataja mafanikio mengine ni kuongeza idadi ya watumishi kutoka 203 hadi 216 kwa mchanganuo wa wanaume 83 na wanawake 133.

"Ndani ya mwaka mmoja wa Rais Samia watumishi 44 chuo kimewapeleka masomoni kati yao 21 wanasoma shahada ya uzamivu,10 wanasoma shahada ya uzamili na 13 wanasoma shahada ya kwanza na wengine 8 wamemaliza na kuripoti kazini kati ya hao 2 wamehitimu shahada ya uzamivu,4 shahada ya uzamili na 2 shahada ya kwanza,"amefafanua

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com