MELI ILIYOBEBA MAGARI 4,000 YA KIFAHARI YAZAMA BAHARINI


Meli ya mizigo iliyokuwa imebeba magari ya kifahari takribani 4,000, imezama katika Visiwa vya Azores nchini Ureno, zikiwa zimepita wiki mbili tangu iliposhika moto.

Meli hiyo iitwayo Felicity Ace, ilikuwa ikisafirisha magari hayo ya kifahari, yakiwemo aina ya Porsches na Bentleys na ilikuwa njiani kuelekea Kisiwa cha Rhode nchini Marekani kutokea bandari ya Ujerumani ya Emden wakati moto ulipozuka.

Wahudumu wote wa meli hiyo waliokolewa wakati moto huo ulipoanza Februari 16.
Joao Mendes Cabecas, nahodha katika moja ya bandari iliyo karibu katika Kisiwa cha Faial, ameliambia Shirika la Habari la Reuters kwamba hakuna uvujaji wa mafuta ulioripotiwa hadi sasa lakini amesema kuna hofu kwamba matenki ya mafuta yanaweza kuharibika wakati chombo hicho kikiwa chini ya Bahari ya Atlantic, katika kina cha mita 3,500.

Jeshi la wanamaji la Ureno limesema hakuna aliyejeruhiwa na moto huo na kwamba wafanyakazi wote 22 wa meli hiyo walipelekwa katika hoteli moja baada ya jeshi la wanamaji, meli nne za wafanyabiashara waliokuwa wakisafiri katika eneo hilo na Jeshi la Anga la Ureno kukamilisha zoezi hilo la kuwokoa.

Kampuni ya kutengeneza magari ya Volkswagen imesema uharibifu wa magari hayo yenye bima unaweza kugharimu karibu dola milioni 155 kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters.

Kampuni ya Bentley ilithibitisha kuwa magari yake 189 yalikuwa ndani ya meli hiyo na kampuni ya Porsche ilisema ilikuwa na magari 1,100 katika meli hiyo.

Mteja mmoja alituma ujumbe wa Twitter akisema kuwa Porsche yake ilikuwa kwenye meli iliyoteketea. Mwingine alituma ujumbe wa Twitter kwamba alikuwa amerudishwa nyuma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post