Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

EWURA YAFAFANUA MWENENDO WA BEI ZA MAFUTA


Meneja Mahusiano  na Mawasiliano EWURA Titus Kaguo akiongea na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu Bei kikomo za bidhaa za mafuta nchini.

Na Dotto Kwilasa-Malunde 1 Blog-DODOMA

MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imetoa bei elekezi kwa bidhaa za mafuta nchini huku ikiweka wazi kuwa bei hizo zingeweza kuwa juu zaidi kama Serikali isingechukua hatua ya kuahirisha tozo ya Shilingi 100 kwa lita kwenye bidhaa za petroli,Dizeli na mafuta ya taa.

Hayo yameelezwa leo jijini Dodoma na Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano EWURA Titus Kaguo wakati akiongea na Waandishi wa habari kuhusu utaratibu wa kila mwezi wa  bei kikomo za bidhaa za  mafuta zitakazoanza kutumika kuanzia Jumatano,2 Machi,2022.

Amefafanua kuwa,Serikali itakuwa inapoteza shilingi Bilioni 30 kwa kila mwezi kutokana na hatua yake ya kupunguza Shilingi 100 kwa kila lita ya mafuta ili kuwajali wananchi.

Akiongea kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA Mhandisi Godfrey Chibulunje ,Kaguo amesema pamoja na kutambua bei hizo,ni muhimu kwa watumiaji kizingatia kuwa bei za rejareja na jumla za mafuta ya petroli,dizeli na mafuta ya taa yaliyopokelewa kupitia bandari ya Dar Es Salaam zimebadilika ikilinganishwa na toleo lililopita la February 2,2022.

"Kwa mwezi Machi 2022 bei za rejareja za petroli na dizeli zimeongezeka Kwa shilingi 69/Lita sawa na asilimia 2.42 na shilingi 65/lita sawa na asilimia 2.77,vile vile bei za rejareja ya mafuta ya taa imepungua Kwa shilingi 83/Lita sawa na asilimia 3.63,"ameeleza Kaguo.

Kadhalika amefafanua kuhusu mwenendo wa bei za mafuta za toleo lililopita kwamba bei za jumla za petroli na dizeli zimeongezeka kwa shilingi 59.65 kwa lita sawa na asilimia 2.54 na shilingi 64.45 kwa lita sawa na asilimia 2.92 mtawalia huku bei ya jumla ya mafuta ya taa ikishuka kwa shilingi 82.67 kwa lita sawa na asilimia 3.82.

"Ni muhimu kujua kuwa mabadiliko yote ya bei yanachangiwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika Soko la dunia ,gharama za usafirishaji na thamani ya shilingi ukilinganisha na dola ya marekani,hivyo bei hizi zitaendelea kupangwa na Soko hilo na EWURA itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za mafuta,"amefafanua

Licha ya hayo amewataka wauzaji wa petroli kutoa risiti za mauzo kutoka kwenye mashine ya EFPP na wanunuzi kuhakikisha wanapata stakabadhi hizo za malipo zinazoonyesha jina la kituo,tarehe,aina ya mafuta yaliyonunuliwa na bei kwa lita na kufafanua kuwa stakabadhi hizo zitatumika kama kidhibiti kwa wanunuzi endapo kutakuwa na kasoro.

"Vituo vyote vya mafuta vinapaswa kuchapisha bei za bidhaa za mafuta katika mabango yanayo onekana bayana na yakionesha bei za mafuta,punguzo,vivutio vya biashara vinavyotolewa na kituo husika,tunawashauri pia wateja kununua mafuta kwenye vituo vinavyouza mafuta bei nafuu zaidi ili kushamirisha ushindani wa soko,"amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com