Mwananchi akichota maji katika mradi wa maji wa kijiji cha Ng'ope kata ya Roche wilayani Rorya
Na Dinna Maningo, Rorya.
WANANCHI wa kijiji cha Ng'ope kata ya Roche wilayani Rorya mkoani Mara wamepata huduma ya maji safi na salama ambayo waliikosa tangu dunia kuumbwa, na wakati wa kiangazi walilazimika kutembea umbali wa km10 kwenda kuchota maji mtoni nchi jirani ya Jamhuri ya Kenya.
Ukosefu wa maji kijijini ulisaababisha baadhi ya wanakijiji kukaa siku mbili bila kuoga,nguo kufuliwa kwa wiki mara moja,kuathiri shughuli zao za kibiashara, utoro shuleni, wanafunzi wengine kuchelewa kwenda shule pamoja na kuibuka kwa migogoro ya ndoa kutokana na ukosefu wa huduma ya maji kijijini.
Hayo yalielezwa na wananchi wa kijiji hicho wakati waandishi wa habari walipofika katika kijiji hicho kutembelea mradi wa maji ili kuona utekelezaji wa ujenzi wa miradi inayojengwa na serikali kupitia wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA) katika wilaya hiyo.
Waandishi waliongozana na maafisa wa RUWASA mkoa wa Mara ambao ni afisa Utumishi Stanley Sing'ira,Eng.Bita Mgema,Meneja RUWASA wilaya ya Rorya, Mhandisi James Kishinhi akiwa na baadhi ya wataamu ili kuwaonyesha miradi inayojengwa, wananchi walieleza adha walizozipata kabla yakupata mradi wa maji wa Ng'ope.
Lucy James alisema kuwa kitendo cha kutembea umbali mrefu kufuata maji nchi jirani ya Kenya alilazimika kukaa siku mbili bila kuoga yeye na familia yake lakini baada ya maji kupatikana sasa wanaoga kila siku.
"Tulikuwa tunaamka saa 12 asubuhi kwenda kufuata maji Kenya unajitwisha ndoo kichwani unatembea kwa mguu umbali mrefu unafika nyumbani ukiwa umechoka sana hata urudie ndoo nyingine ya maji unashindwa,kazi zinakusubiri inabidi ndoo hiyo ya maji itumike kwa ajili ya kupika chakula.
"Ukitoka muda umekwenda unapika unakwenda kibaruani kutafuta pesa unarudi nyumbani muda wa kufuata tena maji haupo unaingia kupika unalala uko hoi kesho yake unaamka kwenda kwenye shughuli zingine bila kuoga maana muda wa kufuata maji hakuna na uwezi kwenda jioni maana utarudi usiku na familia inahitaji uipikie chakula",alisema mwanamke huyo.
Hezboni Elia ambaye ni mwanafunzi wa shule ya sekondari Roche alisema kuwa ukosefu wa maji ulisababisha kwenda shuleni na nguo chafu na baadhi yao kuchelewa shule wengine kutokwenda shule na kubaki kuwasaidia wazazi wao kuchota maji mtoni.
"Maji yalikuwa ya shida sana,siku ya ukaguzi jumatatu ndiyo tulikuwa wasafi kwakuwa siku ya jumapili tulikuwa tunakwenda mtoni kufuata nguo na kuoga, utakaa na nguo hizo wiki nzima siku ya usafi alhamis nguo zinakuwa ni chafu unachapawa kwanini hujafua na ni siku ya usafi,unashindwa kwakuwa ni siku ya shule tunatoka shuleni muda umekwenda huwezi kufuata maji mtoni ni mbali.
"Wanafunzi wengine walichelewa kwenda shule wakiamka asubuhi wanaenda kwanza kufuata maji mtoni ili kuwasaidia wazazi anafika shuleni saa mbili wenzao tayali walishaingia darasani wanakosa baadhi ya vipindi, tunashukuru na shuleni yetu maji yatafika wamechimba ili kuweka bomba.
"Wanafunzi wengine wakiwemo wa shule ya msingi hawakufika shule walibaki nyumbani kulea watoto au kuwapikia maana wazazi wao wanakuwa wamekwenda mtoni kufuata maji nilipokwenda kuchota maji nilijitwisha kichwani kama sikuwa na baiskeri,nilipochoka kutembea nilitua maji chini na kupumzika kisha najitwisha tena naendelea na safari", alisema Hezbon.
"Wengine tulikaa hadi siku tatu bila kuoga kutokana na shida ya maji,unaondoka saa 12 asubuhi unarudi nyumbani saa tano wakati huo unatakiwa kwenda kwenye shughuli zako ukatafute pesa una kosa muda wa kufuata maji mtoni,ukienda kufuata maji kijiji cha Burige asubuhi unakuta foleni ni ndefu unarudi nyumbani saa sita inabidi ubanebane maji unaacha kuoga",alisema.
Vijinia Abuya alisema kuwa ukosefu wa maji uliathiri shughuli za kibiashara na kilimo cha Bustani kwasababu watu walishindwa kufanya biashara zao kwa wakati na badala yake kwenda kutafuta maji.
"Tumepata maji karibu yatatusaidia katika kilimo cha bustani,ulikuwa ukipanda bustani yako ya mbogamboga zinakauka unakosa maji ya kumwagilia,watu ilibidi waache kufanya biashara zao wakatafute maji,ukifuata ndoo moja ukijikaza utarudia maji mara moja tu au ukachote asubuhi ikifika saa tisa ufuate tena ndoo moja,watoto walikuwa wachafu,nguo chafu na unaoga baada ya siku mbili",alisema.
Anastazia Onyango yeye alisema "Ukosefu wa maji ulisababisha tuoshe vyombo mara moja kwa siku ukivitumia asubuhi unavitunza ukishapika mchana ndiyo unavibeba vyote unaenda navyo mtoni kuosha unabeba ndoo ya maji kichwani ukiwa umekalisha na beseni juu ya ndoo lenye vyombo ulivyoosha,wengine walibeba watoto mgongoni kwenda nao kuchota maji,yaani tulichoka sana.
Magreth Jobande alisema kuwa umbali wa kufuata huduma ya maji uliwaathiri watoto wadogo"unaamka saa kumi na mbili asubuhi unarudi saa nne watoto wanachelewa kunywa uji hata watoto wachanga wanaonyonya walikosa haki ya kunyonya kwa wakati mpaka utoke mtoni,watoto wengine walishindwa kwenda shuleni wakabaki kukaa kuangalia watoto.
"Tatizo la maji lilisababisha migogoro kwa wanandoa unatembea umbali mrefu unachelewa kupika mme anagomba umechelewa kumpikia chakula lakini sasa tuna maji unachota unafanya shughuli zako,watoto wanakwenda shule kwa wakati", alisema Magreth.
Edward Moses ambaye ni mwendesha pikipiki maarufu bodaboda alisema kuwa ukosefu wa maji ulisababisha wasioshe pikipiki zao lakini sasa pikipiki ni safi kwakuwa uziosha kila siku baada ya kupatikana kwa maji karibu.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Bondo Paulo Obura aliipongeza serikali kwa kuwasogezea huduma ya maji karibu ambayo ilikuwa kero kubwa huku baadhi ya vitongoji wakiomba maji hayo yasambazwe kwenye vitongoji vyote vya kijiji hicho kwakuwa vitongoji vingine wananchi wanatembea km 4 kufuata maji kitongoji cha senta kulikojengwa mradi wa maji.
"Ni mwezi sasa tangu tupate huduma hii ya maji naishukuru serikali yetu imetatua kilio chetu cha miaka mingi,tulifuata maji mbali Kenya kule Oras au kijiji cha Panyakoo kata ya Goribe tunaomba maji yasambazwe kwenye kitongoji cha Ruore watu wanatembea km 3 kwenda kufuata maji shule ya msingi Ratia, ili ufuate maji senta kuliko na tenki la maji ni km 6", alisema Paulo.
Godfrey Binaisa alisema" Tunaishukuru RUWASA kwakujenga mradi wa maji lakini tunaomba maji yasambazwe kila kitongoji,unamuona huyo anayechota maji anaitwa Oruko Opiyo anakwenda kitongoji cha Bondo km 4 .
Mwenyekiti wa kijiji cha Ng'ope Daniel Amolo alisema kuwa kijiji hicho kina vitongoji vitano ambavyo ni Bondo,Redienya,Okuro,Ruole, na Senta ambako kumejengwa tenki la maji nakwamba kabla ya mradi wananchi wake walifuata maji Kenya au kijiji cha Panyakoo ambayo ni ya lambo yasiyo safi na salama.
"Maji ya lamboni siyo safi na salama hayo hayo uchote unywe humohumo watu wanaogamo,mifugo iingie kunywa maji, tunaishukuru serikali kutupatia mradi wa maji,gharama ya kuchota maji ni sh.50 kwa ndoo moja pesa hukusanywa na zimetunzwa ili kusaidia matengenezo pindi itakapotokea kifaa kimeharibika,hadi sasa kiasi cha sh.150,000 kimekusanywa kati ya fedha hizo 62,000 zimelipa deni la Luku", alisema.
Aliwaomba wananchi kutunza Miundombinu ya maji kwani ukosefu wa maji umewatesa wananchi kwa muda mrefu huku akiiomba RUWASA kusambaza maji katika vitongoji vingine.
Meneja Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA) wilayani Rorya, James Kishinhi alisema kuwa mradi wa maji Ng'ope umeghalimu sh.milioni 198nakwamba vitongoji vyote vya kijiji hicho vitanufaika na mradi huo wa maji.
Mradi wa maji Ng'ope kijiji cha Roche
Mwananchi kijiji cha Ng'ope akichota maji kwenye mradi uliojengwa na RUWASA
Social Plugin