Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NAIBU WAZIRI MARYPRISCA : MIRADI YA MAJI FEDHA ZA UVIKO-19, IKAMILIKE KWA WAKATI


Naibu Waziri wa Maji MaryPrisca Mahundi, akizungumza kwenye mradi wa maji Mkula, mara baada ya kukagua mradi wa Maji Badugu wilayani Busega mkoani Simiyu.
Naibu Waziri wa Maji Maryprisca Mahundi, akitembelea mradi wa maji Nyakabindi, kushoto ni mkuu wa wilaya ya Bariadi Lupakisyo Kapange, pamoja na Mwenyekiti wa Halshauri ya mji wa Bariadi David Masanja (mwenye shati jeupe) ambaye pia ni diwani wa kata ya Nyakabindi, kulia ni Mtendaji wa kata ya Nyakabindi

Na COSTANTINE MATHIAS, Busega.

Naibu Waziri wa Maji Maryprisca Mahundi amewaagiza Mameneja wa Wilaya wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) nchi nzima, kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa kwa fedha za Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi Uviko-19 inakamilika kabla ya mwezi Juni mwaka huu.

Amesema kuwa hakutakuwa na nafasi ya maelezo wala kuongeza muda kwa Meneja yeyote ambaye atashindwa kukamilisha miradi hiyo kwa muda muafaka, ambapo ameagiza miradi yote inatakiwa kukamilika mwezi Mei mwaka huu.

Naibu Waziri huyo ametoa maagizo hayo leo (jana) Mkoani Simiyu, ambapo akiwa Wilayani Busega amemtaka meneja wa Ruwasa wilayani humo anayetekeleza miradi miwili ya Uviko -19 kuhakikisha inakamilika kwa muda.

Amesema kuwa miradi yote ya Uviko-19 mbali na kukamilika ujenzi wake, inatakiwa kutoa maji na wananchi wanaanza kutumia na siyo kukamilika kwa kujengwa tu bali inatakiwa kabla ya muda huo ianze kutoa maji.

Amesema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameleta fedha hizo kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa Uviko, ambapo moja ya njia za mapambano ni wananchi kunawa mikono kwa maji safi na tiririka.


“Kunawa maji safi na tiririka ni lazima kila radi ukamilike ujenzi wake kwa asilimia 100 na siyo kukamilika alafu tunaambiwa kuna kitu fulani hakijakamilika, hapana …tunataka maji yatoke na wananchi waanze kutumia,” amesema Mahundi

“Kwenye hii miradi kama Wizara hatuna Excuse (msamaha) kwa Meneje yeyote wa Wilaya, wala hatuna muda wa ziada kwa ambaye mradi utashindwa kukamilika kwa muda, tunataka miradi ikamilike kabla ya mwezi wa tano na itoe maji kwa wananchi,” ameongeza Naibu Waziri.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji ndani ya Wilaya Busega Meneja wa RUWASA Wilaya hiyo Mhandisi Samson Gagala amesema kuwa walipokea zaidi ya Sh. Milioni 450 fedha za Uviko -19 kwa ajili ya kutekeleza miradi miwili ya maji.


Mhandisi Gagala amesema kuwa miradi hiyo inatekelezwa katika vijiji vya Badugu na Kalemela ambapo ujenzi wake kwa miradi yote miwili umefikia kiwango cha asilimia 25.

“ Kukamilika kwa miradi hii yote miwili itahudumia zaidi ya wananchi 8000, lakini katika Wilaya tunayo mingine ambayo inajengwa kwa fedha za lipa kulingana na matokeo (P4R) zaidi ya Sh. Milioni 900.'' amesema.

Kwa upande wake Meneja Miradi kutoka Jonta Investment Ltd anayetekeleza mradi wa Badugu, Mhandisi Juma Bangula amesema ujenzi wa miundombinu yote utakamilika mwezi huu na kwamba wanatarajia bomba zitafika mwishoni mwa mwezi wa pili.

Ameahidi kuwa watatekeleza mradi huo kwa wakati kwa kuzingatia mkataba na kwamba wananchi pamoja na serikali watarajie kuapata maji kwa wakati.

Musa Ernest mkazi wa Badugu amesema upatikanaji wa maji katika kijiji hicho ni shida na kwamba kukamilika mradi huo utatatua kero ya maji kijijini hapo.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com