Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

UMBALI,FOLENI YA MAJI KISIMANI YAWACHELEWESHA WANANCHI KUFANYA SHUGHULI ZA KILIMO


Mradi wa maji kata ya Bugoji
Meneja RUWASA wilaya ya Musoma Edward Silonga akigusa mashine

Na Dinna Maningo,Musoma
WANANCHI wa kijiji cha Kaburabura kata ya Bugoji wilaya ya Musoma mkoani Mara wanalazimika kutembea umbali zaidi ya km15 kufuata maji kwenye visima vya asili vilivyopo wilaya ya Bunda na wanapofika hukuta foleni ndefu na kujikuta wakichelewa kurudi nyumbani kufanya shughuli zao za kilimo.

Hali hiyo inaelezwa kuwa inawakwamisha kufanya kazi za nyumbani na kilimo kwa wakati kwakuwa kijiji chao hakina huduma ya maji safi na salama,wanatumia maji ya madimbwi waliyoyachimba wenyewe ambayo wakati wa kiangazi hukauka.


Wakizungumza na waandishi wa habari kijijini hapo waliotembelea miradi ya maji inayojengwa na wakala wa maji na usafi wa mazingira (RUWASA) katika wilaya hiyo,wananchi walieleza changamoto ya maji na kusema kuwa mradi wa maji ukikamilika utawaokolea muda wa kufanya shughuli za kilimo.


Mkazi wa kijiji hicho cha Kaburabura Mariamu Bumbasi alisema kuwa wanatembea umbali mrefu zaidi ya km 15 kwenda kuchota maji kijiji cha Kangetutya kilichopo wilaya ya Bunda na wanapofika huko hukuta watu wengi na hivyo kuchelewa kurudi nyumbani.


"Wakati wa kiangazi tunateseka sana unaamka saa tisa kwenda kutafuta maji unatembea masaa mawili ukifika huko unakuta watu wengi foleni ni ndefu mnapanga ndoo zenu kusubiri hadi ifike saa mbili za asubuhi mwenye kisima ndiyo aje afungue kisima mchote" alisema 


Mariamu alisema kuwa pamoja na umbali mrefu wanapofika kisimani wanachota maji kwa saa chache nakisha kufungwa na kufunguliwa tena saa kumi jioni jambo ambalo linawafanya wawahi maji na kuacha kufanya kazi za shamba.


"Kuna ratiba za kuchota maji saa mbili asubuhi hadi saa tano ikifika huo muda kisima kinafungwa kuchota ni saa kumi jioni yaani hata ukiwahi kisimani mtapanga foleni kusubiri huo muda ufike ndiyo mchote maji, sisi tusio na baiskeri tunatembea kwa miguu unawahi asubuhi na ndoo yako moja unakwenda kuchota maji ukienda saa 12 asubuhi kurudi ni saa nne.


"Ikifika mida ya saa nane mchana mnaanza safari kwenda kisimani mkifika mnapanga foleni saa kumi kisima kinafunguliwa wewe una ndoo moja ya maji unakaa kusubiri foleni wenzako wa karibu na kisima wana ndoo hata sita na wa baiskeri wana madumu mengi wachote wamalize ifike zamu yako uchote ndoo yako moja uondoke unachelewa kufika nyumbani kutokana na umbali na na wingi wa watu kisimani yaani akina mama tunateseka sana", alisema Mariamu


Sara Ramadhani alisema kuwa maji ya dimbwi wanayotumia si safi na salama ni machafu hali inayosababisha baadhi ya watu kupata maradhi ya tumbo na kichocho.

"Maji tunayochota kwenye madimbwi ni machafu kiasi kwamba hata uso unashindwa kunawa,hayo hayo ndiyo tunachota,ng'ombe wanakunywa humohumo mbwa,watu wanaugua matumbo,huwa tunafata maji kule Kangetutya tunalipa 2,000 kwa mwezi hiki kijiji kina changamoto kubwa ya maji hata mifugo iliwahi kufa kwa kukosa maji", alisema Sara.


Sikujua Mjora alisema kuwa kutokana na shida ya maji hufua nguo moja yakutokea nakwamba ukosefu wa maji unasababisha wasiweze kupariria kwa wakati mashamba yao ya mihogo.


"Maji ni ya shida unayochota hayatoshi ukitaka kutoka unafua nguo moja uvae utoke,pia muda ambao ungewahi shambani unawahi kwenda kupanga foleni kusubiri maji,tukipata huu mradi wa maji utatusaidia maana tutafanya kazi zote kwa wakati unaenda shambani ukitoka una raha unajua maji yapo karibu utachota, tunashindwa kwenda kupariria mihogo kisa kwenda kutafuta maji,sisi ni wakulima pia wa mahindi,viazi vitamu,mpunga na mtama", alisema Sikujua.


Diwani wa kata ya Bugoji Ibrahimundi Buruya aliishukuru serikali kuipatia kata hiyo mradi wa maji safi na salama ambao utasaidia kupunguza changamoto nakwamba tatizo la ukosefu wa maji uliwatesa kisiasa pindi walipokuwa wakijinadi kutafuta kura.

"Kijiji cha Kaburabura wameteseka sana wengine walifata maji kijiji cha Guta kilichopo Bunda umbali wa km 28, mradi wa pesa za uviko utasaidia ambapo tayali vituo 20 vimewekwa ili watu wapate maji na tuna matenki mawili maji yatasambazwa vijiji vyote kwakweli tunamshukuru sana Rais wetu mama Samia kaokoa watu wa vijijini", alisema.


Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Edward Silonga alisema kuwa katika mwaka wa fedha  Serikali imetoa fedha Bilioni 2.199 kutekeleza miradi saba ambapo kata ya Bugoji ina matenki mawili yenye ujazo wa lita 200,000 kila mmoja itakayotoa huduma ya maji katika vijiji vya kata hiyo na kwamba miradi yote itakamilika ifikapo Juni,2022.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com