Wizara ya Maji imeitaka Kampuni iliyopewa zabuni ya kusambaza mabomba kwenye ujenzi wa miradi ya maji Kanda ya Ziwa inayotekelezwa na Serikali kupitia fedha za Uviko 19, kuhakikisha inafikisha mabomba hayo kwa wakati kwenye maeneo ya miradi, ili kuepuka kukwamisha miradi hiyo na hatimaye lengo la Serikali la kuwafikishia wananchi maji safi na salama liweze kufikiwa.
Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi ametoa rai hiyo wakati akikagua mradi wa maji wa Bunamala Mbugani wilayani Itilima mkoani Simiyu na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo.
Amesema katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Uviko 19, ni lazima wananchi wahakikishiwe upatikanaji wa maji safi na salama ambayo yatawasaidia kujikinga na maradhi hayo.