Diwani kata ya Sirari Amos Sagara akionesha kisima cha kukusanyia maji kilichojaa na kusababisha maji kumwagika
Diwani kata ya Sirari Amos Sagara akimtwisha ndoo mwanafunzi
Akina mama wa kijiji cha sokoni kata ya Sirari wakichota maji kwa furaha baada ya mradi kukamilika na kutoa maji
Mradi wa maji Sirari
****
Na Dinna Maningo, Tarime
WANANCHI wa kijiji cha Buriba kata ya Sirari wameiomba serikali kuipatia fedha Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) za kujenga tenki jipya la maji ili kuyanusuru maji yanayomwagika kutokana na kisima kinachokusanya maji (Sump Well) kuzidiwa uwezo wa kuhifadhi maji.
Kijiji hicho kina kisima kimoja kinachokusanya maji yanayotoka kwenye kisima cha asili kisha kwenda kwenye tenki kubwa la mradi wa maji Sirari linalohifadhi maji lililopo katika kitongoji cha Mlimani ambalo tayali wananchi wameanza kupata huduma ya maji.
Wakizungumza na Waandishi wa Habari waliofika katika kijiji hicho kutembelea Mradi wa maji wa Sirari unaotoa huduma ya maji kwa wananchi,Wanakijiji walisema kuwa kabla ya mradi huo wakati wa kiangazi walichota maji kwenye visima viwili vya asili ambavyo ni kisima cha Kemogere na Bunchanga.
Jane Manga mkazi wa kijiji cha sokoni alisema kuwa kabla ya mradi wa maji kujengwa nyakati za kiangazi walihangaika kupata maji lakini baada ya mradi huo umesaidia kuwapunguzia mwendo kwenda kutafuta maji kijiji cha Buriba.
"Mradi utahudumia vijiji vinne kata ya Sirari na vijiji jirani,kabla ya huu mradi ilipofika wakati wa kiangazi maji yalipatikana kwa shida tulinunua kwenye visima vya watu binafsi,ndoo moja sh.100 au utembee km.2 kufuata maji kwenye visima vya asili, kwa sasa tunayapata kwa sh.50 kwa ndogo moja'
Edina Martini alisema kuwa baada ya kujengwa tenki linalohifadhi maji wamepata unafuu kwasasa hawatembei umbali mrefu kutafuta maji,lakini kisima kimejaa.
" Kisima kimejaa maji yanamwagika bure yanaenda Kenya wakati kuna baadhi ya vitongoji havijapata maji ambavyo vingepatiwa maji hili kuyaokoa haya maji yanayomwagika bure.
Diwani wa kata ya Sirari Amos Sagara alisema kuwa awali kabla ya mradi maji mengi kutoka kwenye vyanzo vya maji yalimwagika na kutiririka kwenda Kenya,hali iliyosababisha waombe mradi wa maji kunusuru upotevu wa maji.
" Kisima kimejaa tunaomba serikali kupitia RUWASA watoe fedha lijengwe tenki lingine,tuliamua kutoa visima vya asili ili visaidie huduma ya maji baada ya kuona maji mengi yanatiririka kwenda Kenya, wataalamu wa RUWASA wakaja wakakijengea kisima ili kuzuia maji kutiririka kwenda Kenya,wametengeneza tenki la maji lakini tatizo la upotevu wa maji halijaisha.
"Haya maji ni ya asili na yalipimwa na wataalamu yakathibitishwa yana ubora hayahitaji hata kuwekewa dawa,kuna vitongoji havina maji tunaomba haya maji yanayomwagika bure litengenezwe tenki lingine la kupokea maji ili yasambazwe kwenye kitongoji vingine kusaidia adha ya maji inayowapata wananchi wanaoishi kwenye vitongoji ambavyo vina changamoto ya maji" alisema Sagara.
Akizungumzia mradi wa maji Sirari,Sagara alisema kuwa ujenzi wa mradi ulianza mwezi juni,2021 na umekamilika,mwezi januari,2022 ulianza rasmi kutoa huduma ya maji kwa wananchi.
"Awali mradi huu wakati unafanyiwa upembuzi ulikisiwa kujengwa kwa sh.Bilioni 1.2 lakini RUWASA walipofanya upembuzi bajeti ilipungua,mradi umejengwa kwa kiasi cha fedha Milioni 534 kati ya fedha hizo Milioni 460 zimetumika na maji yamepatikana.
" Sirari ina wakazi wengi zaidi ya 60,000 tunaomba fedha ziongezwe za kuwezesha kusambaza maji kwenye vitongoji vyote kwakuwa lengo la kujenga mradi huu ni kuzifikia kata tatu,Sirari,Regicheri na Gwitiryo.
Sagara na wananchi wengine akiwemo Jeni Maga wanamshukuru Rais Samia Suluhu kuwezesha upatikanaji wa huduma ya maji ambapo fedha nyingi zimetolewa na serikali kutekeleza miradi mingi ya maendeleo ikiwemo miradi ya maji ambapo huduma ya maji imekuwa ni changamoto lakini kwa sasa kuna unafuu kwakuwa miradi ya maji imejengwa na mingine inaendelea kujengwa.
Deogratius Mwita anayekusanya fedha wananchi wanapofika kuchota maji kwenye mradi huo alisema kuwa umesaidia kuondoa kero ya maji ambapo kila siku upata mauzo ya maji kati ya sh.15,000-25,000 na hadi sasa fedha zipatazo 760,000 zimekusanywa zipo benki na mwezi januari wamelipa Luku sh.505,000 ya umeme.
"Maji ni mengi ukiona hayatoki kwenye mabomba labda ukute luku imeisha maana haya maji yanasukumwa kwa umeme luku ikiisha wanaweza kukaa siku moja bila maji alafu pesa inalipwa watu wanapata maji" alisema Mwita.
Mhasibu wa mradi wa maji kata ya Sirari Adventina Itira alisema kuwa baada ya kujengwa mradi huo sasa wananchi ndiyo wasimamizi wa mradi"mradi upo chini ya jamii pesa inayokusanywa ni kwaajili ya kutekeleza mahitaji mbalimbali ya mradi,pesa za maji ndizo zinamlipa mlinzi wa mradi anaepokea asilimia 10 ya fedha anazokusanya wakati watu wanapofika kununua maji.
Mbunge wa jimbo la Tarime vijijini Mwita Waitara alisema kuwa mradi wa maji Sirari utawanufaisha wananchi ambao awali waliteseka kupata huduma ya maji lakini anaiomba serikali kuongeza tenki lingine kwakuwa lililopo limezidiwa maji yanapotea bure licha ya kwamba maeneo mengine yanahitaji kufikiwa na huduma ya maji.
Meneja Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wilaya ya Tarime Mhandisi Malando Masheku akiwa ameambatana na baadhi ya wataalamu wa RUWASA na wa Idara ya Maendeleo ya jamii katika wilaya hiyo, alisema kuwaTenki wanaloomba kupatiwa fedha ni ambalo limejengwa Mlimani lenye ujazo wa lita 150,000 na siyo kisima cha kukusanyia maji kutoka kwenye chanzo cha maji chenye ujazo wa lita 135000.
"Maji yanamwagika kwa sababu hakuna Tenki la kuyapokea,hapo ndiyo kuna pampu ya kusukuma maji,kungekuwa na Tenki pampu ingesukuma maji lakini hawakuwasha kwa sababu lile la Mlimani lilikuwa limejaa.
"Mradi wa Sirari tenki lina ujazo wa lita 150,000 ambapo kazi zilizopangwa ni uchimbaji wa visima vitatu,ujenzi wa mfumo wa umeme,ununuzi na ufungaji wa pamp 3,ununuzi wa bomba,uchimbaji wa mtaro na uflazaji wa bomba na ufukiaji wa mtaro 11.503km,ujenzi wa vituo 15 (DPs),ujenzi wa viosk 8 na ukarabati wa bears kwa kuondoa matope na kuboresha tuta" alisema.
Masheku alisema kuwa utekelezaji uliofanyika hadi sasa ni uchimbaji wa visima vitatu(kusoma kimoja ndicho kilipata maji lita 4,000 kwa saa,viwili maji hayakupatikana,uunganishaji umeme wa gridi ya Taifa,ununuzi na ufungaji wa pampu,ununuzi wa bomba,uchimbaji wa mtaro (km 14),ulazaji wa bomba (km 13) na ufukiaji wa mtaro.
Aliongeza kuwa muda uliopangwa kukamilika kwa ujenzi ni tarehe 20,Aprili ,2022 nakwamba mradi huo hadi kukamilika utagharimu Milioni 534,unatoa huduma ya maji kwa wananchi na upo katika hatua ya ukamilishaji.
Social Plugin