Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu, leo Machi 4, 2022 wamefutiwa mashtaka yote yaliyokuwa yakiwakabili katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.
Mbowe na wenzake wameachiwa baada ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali, DPP, kuwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea na shauri hilo.
Mbali na Mbowe, wengine ni Adam Kasekwa, Halfani Bwire na Mohamed Ling’wenywa waliokuwa makomandoo wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando ameieleza Mahakama kwamba, “Mkurugenzi Wa Mashitaka (DPP) kwa niaba ya Jamhuri anaomba kuwasilisha taarifa ya kutokuwa na nia na kuendelea na shauri hili.”
Amesema, taarifa hiyo tunaitoa chini ya Kifungu cha 91(1) kwa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Mawakili wa utetezi, wakiongozwa na Kiongozi wa Jopo la Mawakili wa Utetezi, Peter Kibatala walidai hawana pingamizi juu ya ombi hilo na kuiachia mahakama.
Nje ya viunga vya Mahakama, shangwe zimetawala kwa baadhi ya wanachama wa Chadema waliojitokeza kusikiliza kesi hiyo.
Hata hivyo, Mbowe na wenzake hawakuwepo mahakamani wakati kesi hiyo ikifutwa.
Social Plugin