Mwanasiasa Mkongwe nchini Tanzania Khamis Mgeja
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mzalendo Foundation, inayojishughulisha na Utawala Bora, Haki na Demokrasia Khamis Mgeja amesema ndani ya mwaka mmoja Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha uwezo mkubwa wa kiuongozi na uliojaa ukomavu mkubwa wa kisiasa na maono makubwa, hekima, busara na karama.
Akiongea na Waandishi wa Habari ofisini kwake Machi 16,2022 Mjini Kahama alipokuwa anazungumzia Mwaka mmoja wa uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, Mgeja amesema Rais Samia ni kiongozi shupavu aliyeandalika mwenye upendo na wananchi wake, aliyeshiba dini na hofu ya mwenyezi Mungu anayechukia dhuluma na kuona haki inasimama.
“Watanzania wakati tunatimiza mwaka mmoja tukiongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan yapo mengi tuliyoona na tuliyosikia na kujifunza kutoka kwake ili kuyafanyia tathmini na kuyawekea mazingatio. Jambo moja kubwa watanzania kwanza tunalotaka kupaswa kujifunza na kujua historia ya nchi yetu ya Tanzania na hasa nchi zinazofuata siasa za ujamaa na kujitegemea katika mifumo yake halisi ya kupata viongozi ambao ni utamaduni uliojengeka kwa miaka mingi ili yawe mazingatio kwa siku za leo na zijazo”,amesema Mgeja.
“Kabla hatujazungumzia uongozi shupavu uliotukuka wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan tuanze kwanza kwa kujikumbusha historia za nchi zote za kikomonisti, mfumo wake mkuu wa kupata viongozi wazuri kwanza viongozi huandalika kuwa viongozi wazuri na wenye kuzingatia maadili ya kiutumishi na uongozi wa umma”,amesema.
Mgeja ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga amesema nchi za kijamaa na Tanzania ikiwemo zinao mfumo wake rasmi wa kupata viongozi wazuri na hasa walioandalika kiuongozi akitahadharisha mkiuacha tu mfumo au kuusaliti kwa kutopata viongozi walioandalika dhambi yake lazima iwatafune waliokuwemo na wasiokuwemo pamoja na nchi kwa ujumla lazima itikisike.
“Uongozi wa nchi yetu kuwa umepata bahati kubwa sana hivi sasa ya kupata kiongozi aliyeandalika ambaye ni Mhe. Samia Suluhu Hassan ni ukweli usiopingika nchi ikipata kiongozi aliyeandalika inatulia tuli kama maji ya mtungi mnabaki kuongelea jinsi gani ya kujiletea maendeleo kwa haraka na kuuweka mstakabali wa nchi kuwa mzuri kwa nyanja zote za kisiasa na kiuchumi”,ameeleza Mgeja.
“Ukitaka kujua kiongozi ni yupi na ni wa aina gani, ni yule unayemuona kiongozi anayetoa uongozi mzuri, Mama yetu Mhe. Samia Suluhu Hassan ni kiongozi mzuri anayetoa uongozi na kuonyesha njia na maono yake kwa wale anaowaongoza”,ameongeza.
Mgeja pia amewakumbusha Watanzania maneno ya Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliyowahi kusema tukitaka kuendelea tunahitaji mambo manne ambayo ni Watu, Ardhi ,Siasa Safi na Uongozi bora.
“Katika uongozi wa awamu ya sita (6) chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, Falsafa hizo za baba wa Taifa tunaona ambavyo anazifanyia kazi vizuri sana na ni imani yetu tuko vizuri na tunaendelea vizuri kimaendeleo. Chini ya uongozi wake imara na shupavu kwa mwaka mmoja watanzania ametuweka wamoja bila kujali dini, ukabila, ukanda, siasa na jinsia”, amesema Mgeja.
“Pia kazi kubwa njema ameshirikisha uongozi wake na makundi mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, wanasiasa, machifu, wafanyakazi na wakulima, wafanyabiashara na machinga, wanamichezo na wasanii, pia makundi mbalimbali yakiwemo makundi ya vijana,watu wenye ulemavu, aakina mama na wazee”,amesema.
Amefafanua kuwa katika uongozi wake wa mwaka mmoja wa Rais Samia Watanzania wanaishi kwa matumaini makubwa pia yaliyojaa faraja lakini mahusiano ya Tanzania na nchi mbalimbali duniani kibiashara na kidiplomasia yamerejea na yanaendelea kukua kwa kasi kubwa na kuindoa nchi katika dhana iliyotaka kujengeka kuwa ni Kisiwa.
“Chini ya uongozi wa Rais Samia Muungano wetu umeendelea kuwa imara hata swala la ulinzi na usalama Rais wetu kama Amiri Jeshi mkuu kwa mwaka mmoja watanzania wanaishi kwa amani na usalama wakifanya kazi zao za kujiletea maendeleo hiyo ndio agenda kubwa namba moja, kama hakuna amani maendeleo hayatakuwepo na wawekezaji hawatakuja kuwekeza Tanzania. Mungu ibariki Tanzania, Mungu Mbariki Rais wetu Mh. Samia Suluhu Hassan”, amesema Mgeja.
Mgeja amewaomba watanzania wote bila kujali dini, kabila, ukanda na wanasiasa wote kumuombea na kumuunga mkono Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ili aendelee kulitumikia Taifa la Tanzania vizuri na kujiletea maendeleo akibainisha kuwa ana imani mpaka mwaka 2025 nchi itapaa kimaendeleo.
Social Plugin