Karolina Bielawska (23) kutoka Poland, ameshinda taji la shindano la urembo la dunia ‘Miss World 2021’.
Karolina amepokea taji hilo kutoka kwa Toni-Ann Singh kutoka Jamaica, mrembo aliyeshikilia taji hilo kwa muda mrefu zaidi katika historia ya shindano hilo la urembo duniani.
Mshindi wa pili wa Miss World 2021 ni Shree Saini kutoka Marekani na mshindi wa tatu ni Olivia Yace kutoka Ivory Coast.
Shindano hilo kubwa la urembo duniani kwa mwaka huu limefanyika katika ukumbi wa muziki wa Coca-Cola ulioko San Juan huko Puerto Rico.
Hapo awali shindano hilo la Miss World lilipangwa kufanyika Desemba 16 mwaka 2021 katika ukumbi wa José Miguel Agrelot Coliseum, lakini baadaye liliratibiwa upya na kupangwa kufanyika Machi 16, mwaka huu.
Mabadiliko hayo yalitokana na janga la UVIKO -19, ambapo nchi nyingi duniani zilikumbwa na janga hilo.
Warembo 40 kutoka nchi mbalimbali duniani walishiriki katika kinyang’anyiro hicho, ambapo 13 kati yao walifanikiwa kuingia 13 bora.
Warembo walioingia 13 bora ni Đỗ Thị Hà wa Vietnam, Karolina Vidales wa Mexico, Anna Leitch wa Ireland Kaskazini, Tracy Perez wa Ufilipino na Karolina Bielawska wa Poland.
Wengine ni Khadija Omar wa Somalia, Shree Saini wa Marekani, Andrea Aguilera wa Colombia, Karolina Kopincova wa Jamhuri ya Czech, April Benayoum wa Ufaransa, Manasa Varanasi wa India, Carla Yules wa Indonesia na Olivia Yace kutoka Ivory Coast.
Social Plugin