Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAKAMPUNI YA KITANZANIA KUWEZESHWA KUPITIA PROGRAMU YA KUENDELEZA BIASHARA ZA WAZAWA INAYOTEKELEZWA NA MGODI WA DHAHABU WA NORTH MARA


Wahitimu wakiwa katika picha ya pamoja
***
Kampuni ya madini ya Barrick Gold Corporation imetangaza kuwa makampuni 15 yamehitimu kutoka kwenye progamu ya kuendeleza biashara za ndani.

 Tangu kuanzishwa kwa programu hiyo mwezi Novemba mwaka 2021, makampuni ya ndani ya nchi yamepatiwa mafunzo mara nne kwa nyakati tofauti katika kipindi cha miezi minne kwa lengo la kujenga uwezo na kusaidia makampuni yaweze kunufaika na fursa zilizopo kwenye sekta ya madini.

Programu hii imefadhiliwa na Kampuni ya Barrick na imetekelezwa na kampuni ya Kengo kwa kushirikiana na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na imekuwa ikitoa mafunzo ya kitaalam na ushauri wa kibiashara kwa makampuni madogo na ya kati ili kuziimarisha kiujuzi na kuziwezesha kunufaika na mnyororo wa thamani wa sekta ya madini. 

Rais na Mkurugenzi Mkuu wa Barrick, Mark Bristow amesema kuwa programu hiyo ni ya kwanza na kipekee kwenye sekta ya madini na amewasihi wengine kufuata mfano huo.

“Tunajivunia kwa kuongoza njia kwa kufanikiwa kuendesha program hii ya maendeleo ya biashara za ndani ya nchi na tumetimiza wajibu zaidi ya sheria zilizopo maudhui ya ndani. Maudhui ya ndani ni muhimu kwa shughuli zetu na tunapoziimarisha kampuni ndogo na za kati, tunaziimarisha na jamii zinazotuzunguka. Barrick itaendelea kuunga mkono maendeleo ya kampuni ndogo na za kati ambazo ni muhimu sana katika ukuaji wa uchumi,” alisema.

Program hii imeshuhudia mafanikio makubwa kama vile utengenezaji wa mipango mikakati kwa ajili ya makampuni yanayoshiriki, kuimarishwa kwa mzunguko wa fedha na uunganishwaji wa fursa mbalimbali za kibiashara.

Wahitimu pia wameweza kunufaika na mafunzo kutoka Wizara ya Madini, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), washauri wa rasilimali watu, na taasisi za kifedha.

 Shack Noels kutoka kampuni ya EHS Company Limited amesema kuwa programu hiyo imeitambulisha biashara yake kwenye viwango vya kimataifa vya utendaji jambo linalomlazimu kuboresha ubora wa huduma zake za ukandarasi. 

Kupitia mafunzo baina ya mkufunzi na mshiriki, makampuni hayo yameweza kuungana na mtandao wa ikolojia ya uchimbaji madini na kutambua maeneo ya ukuaji.

Janeth Reuben Lekashingo, Kamishna wa Kamisheni ya Madini amesema: Serikali kupitia Kanuni ya Kushirikisha Wananchi katika Mnyororo wa Uchumi wa Madini ya Mwaka 2017 imetoa mfumo wezeshi kwa ajili ya biashara za ndani ili zinufaike kutoka kwenye uwekezaji unaofanywa nchini kupitia fursa zilizopo kwenye mnyororo wa thamani.

 Aidha, Program ya Kuendeleza biashara za ndani wa Mgodi wa Dhahabu North Mara umeweka viwango ambavyo makampuni mengine yanaweza kufuata.

Halfa ya mahafali hayo ilihusisha wageni waalikwa wakiwemo wakufunzi, Maafisa wa Serikali, Taasisi za Kifedha na Wabia katika Sekta ya Madini.

Kamishna wa Tume ya Madini, Janeth Reuben akiwahutubia wahitimu na wageni waalikwa wakati wa mahafali hayo.
Wahitimu na wageni waliohudhuria hafla hiyo wakifuatilia matukio.
Kamishna wa Tume ya Madini, Janeth Reuben akikabidhi cheti kwa Mwenyekiti wa Kikundi cha vijana cha Wings Yusuph Gesase wakati wa mahafali hayo.
Mmoja wa wahitimu Judith Mweta, kutoka kampuni ya Gree Culture TZ Ltd, akipokea cheti kutoka kwa Kamishna wa Tume ya Madini, Janeth Reuben (Kulia)
Mkuu wa wilaya ya Tarime Kanali Michael Mtenjele, akiongea na wahitimu na wageni waalikwa wakati wa mahafali hiyo.
Meneja wa Mahusiano wa Kijamii wa Barrick North Mara Gilbert Mworia, akiongea na wahitimu na wageni waalikwa wakati wa mahafali hiyo
Baadhi ya wahitimu wakibadilishana mawazo wakati wa hafla hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com