Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUIPATIA NHC BIL. 173.9 KUENDELEZA MIRADI ILIYOKWAMA

 

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Allan Kijazi 
Baadhi ya nyumba za NHC -Iyumbu Dodoma zikiwa zimekamilika tayari Kwa kuwauzia wateja wake ambapo nyumba moja inauzwa kuanzia milioni 58 hadi 100 zikiwa zimejengwa kisasa kukidhi mahitaji

Na Dotto Kwilasa-Malunde 1 Blog -DODOMA .

SERIKALI kupitia Wizara ya Ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi imesema ina mpango wa kukarabati nyumba za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) huku ikitoa nafasi kwa Shirika hilo kukopa bilion 173.9 kwa ajili ya kukwamua miradi iliyokwama katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Hayo yameelezwa leo jijini hapa na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Allan Kijazi katika kikao chake na Waandishi wa habari  na kueleza kuwa NHC  limeidhinishiwa na hazina mkopo wa  shilingi bilion 44.7 ili kuendelea kazi ya kuifufua miradi hiyo.

Dk. Kijazi ameitaja miradi iliyokwama kuwa ni pamoja na mradi wa Kawe 711, Morocco Square na mradi wa Plot 300 regent Estate iliyopo Dar es salaam.

"Ntakuwa mchoyo wa fadhira kama sitatoa shukrani za dhati kwa serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuliamini Shirika la Nyumba la Taifa na kulipa miradi mikubwa katika maeneo mbalimbali nchini  ikiwemo ile ya kimkakati,"amesema.

Kuhusu mradi wa nyumba 1,000  unaotekelezwa na NHC Dodoma Dk. Kijazi amesema serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitoa mkopo nafuu wa sh. bilion 20 kwa shirika ili zitumike kama mtaji  ambao utatekelezwa kwa miaka 15.

Amesema mkopo huo utalipwa kwa miaka 12  baada ujenzi wa mradi wa nyumba 1,000 kukamilika  ambapo adhma ya serikali ni kuwezesha Shirika kujenga nyumba Dodoma ili kurahisisha upatikanaji wa makazi baada ya serikali kuhamishia shughuli zake.

"Fedha za mkopo nafuu wenye riba ya asilimia 6.75 zimetolewa na serikali kupitia benki ya Azania ambayo imekubali kuwakopesha wanunizi wa nyumba za iyumbu kwa riba ya asilimia 9 ambapo kupitia fedha zitakazopatikana baada ya kuuza nyumba hizo 1,000 zitalisaidia Shirika kupata fedha na  kujenga nyumba nyingine,"amesema

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa NHC Dk. Maulid Banyani alisema shirika liliendesha operesheni maalumu Kwa wadaiwa sugu ambapo  ilisaidia Shirika kukusanya sh. bilion 5 kati ya 27 inazodai kutoka Kwa wateja wake.

Amesema operesheni hiyo itakuwa endelevu na sasa wanakuja na mfumo maalumu ambao utakusanya kodi kwa njia ya kisasa na mfumo huo upo katika majaribio katika nyumba za chamwino.

"Tunaendelea kutoa rai kwa wamiliki wa nyumba zetu kuhakikisha wanalipa kwa wakati na Kwa wale ambao wanauza nyumba zetu pia tunaendesha operesheni na hadi sasa tumeshawakamata watu 30 ambao walitaka kuzifanyia biashara,"amesema.

Kuhusu mradi wa Kawe 711 Dk. Banyani amesema tayari mkandarasi yuko saiti anaendelea na kazi ndogo ndogo .

Naye Meneja Mradi wa NHC Frank Mambo anayesimamia ujenzi wa nyumba 1,000 katika eneo la Iyumbu na chamwino alisema mradi huo umesaidia kupatikana kwa ajira 600 ambazo ni kwa mafundi ujenzi vibarua, wasambazaji, wauzaji vifaa,mama lishe,walinzi na magari ya kusafirisha mizigo.

Amesema mradi huo utagharimu sh.bilioni 71 hadi kukamilika kwake na kufafanua kuwa katika awamu ya kwanza yenye nyumba 404  itagharimu sh.bilion 21.4 huku ukiwa unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi mei mwaka huu na kueleza kuwa awamu ya pili itahusisha ujenzi wa nyumba 325 na majengo sita ya kutoa huduma na awamu ya tatu itahusisha ujenzi wa nyumba 275.

"Nyumba 101 zinazojengwa chamwino ni kwa ajili ya kupangisha na 303 za iyumbu zitauzwa kwa wananchi wanaohitaji nyumba hizi zipo za aina tatu ambazo ni mita za mraba 75 zipo 50,mita za mraba 100 zipo 100 na nyumba zenye mita za mraba 120 zipo 150,"alieleza

Amesema shirika hilo linatekeleza ujenzi wa mradi huo kwa kutumia watalaam wa ndani katika kazi za kuandaa michoro, kukadilia gharama,kusimamia na ujenzi.

Aidha, ameeleza kuwa ili kuwawezesha watakaokuwa wakaazi wa nyumba hizo,kupata huduma muhimu, maeneo yote ya ujenzi wa nyumba za awamu ya kwanza Iyumbu yamewekewa huduma za muhimu ikiwemo maduka, eneo la burudani na shule ya awali, maeneo ya michezo na sehemu za kuabudia. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com