KUPITIA kituo cha runinga cha Fox News, Seneta wa Marekani, Lindsey Graham amesababisha hasira kwa baadhi ya raia wa Urusi baada ya kuwataka watu wa Urusi kumuua rais wao, Vladimir Putin.
Graham kutoka Chama cha Republican katika Jimbo la South Carolina, amenukuliwa akisema: “Njia pekee ya uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine kuisha ni kwa mtu nchini Urusi kumuua Putin, atakuwa ameifanyia nchi yake na ulimwengu kazi nzuri sana.”
Kauli hiyo imezua hasira na kusababisha balozi wa Urusi nchini Marekani, Anatoly Antonov, kuomba maelezo juu ya matamshi hayo ambayo ameyaita kuwa ni matamshi yasiyokubalika na ya mauudhi.
Mzozo wa Urusi na Marekani bado unaendelea huku asilimia kubwa ya Jeshi la Urusi likiwa tayari limeshaingia nchini Ukraine na linatekeleza mashambulizi katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Zaidi ya raia 2,000 wa Ukraine wameshathibitishwa kupoteza maisha huku watu zaidi ya milioni moja wakikimbia taifa hilo ili kuokoa maisha yao.
Mataifa mbalimbali ya Ulaya na Marekani yamekuwa yakipinga vikali vita hivyo yakisema uvamizi wa Putin nchini Ukraine ni ugaidi huku wakimtaka aondoe jeshi lake nchini humo mara moja. Wakati huo huo Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky yeye ameomba maridhiano ili kumaliza mzozo huo.
Social Plugin