UWT NJOMBE YAPONGEZA KASI YA RAIS SAMIA...KEVELA ASEMA 'ANAUPIGA MWINGI'

 MWENYEKITI wa Jumuiya ya Umoja wa wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Njombe Scolastika Kevela  (pichani) amempongeza Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipaisha Tanzania kimaisha.

Akizungumza mkoani humo, Kevela amesema chini ya uongozi wa Rais Samia, Tanzania inapiga hatua kubwa kimaendeleo kwa kukaribisha idadi kubwa ya wawekezaji na watalii sambamba na kukuza ushirikiano kimataifa jambo ambalo limezidi kulitangaza jina la Tanzania ulimwenguni.


Kauli ya Mwenyekiti huyo imekuja siku chache baada ya Rais Samia kushuhudia kusainiwa kwa mikataba 36  ya makubaliano (MoU)nchini Dubai inayogusa sekta mbalimbali yenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni7.4 sawa na Sh Trilioni 17. 35.


Mikataba hiyo inayohusisha sekta za nishati, kilimo, ujenzi, anga, mawasiliano,habari na biashara, imesainiwa nchini Dubai katika mkutano wa kimataifa na kushuhudiwa na Rais Samia ambaye pia alipata nafasi ya kuhutubia katika maonyesho ya ‘Dubai Expo 2020’ yanayofanyika nchini humo.


“Napenda kutumia nafasi hii kumpongeza kwa dhati Rais Samia Suluhu kwa kuzidi kutupaisha watanzania kiuchumi na kimaendeleo, ndani ya uongozi wake wa muda mfupi wa mwaka mmoja amefanya makubwa kiasi cha kuwafanya watanzania wengi kufurahia uongozi wake, sisi kama wanawake wa mkoa wa Njombe tuahidi kuwa naye bega kwa bega”, amesema Mama Kevela


Ameongeza kuwa hatua ya Rais Samia kuiwezesha Tanzania kwenda kushiriki kwa mara ya kwanza na kuwa na banda lake katika maonyesho hayo nchini Dubai tangu ipate Uhuru, kimeitangaza Tanzania kimataifa na zaidi kitaongeza idadi ya wawekezaji na watalii watakaokuja nchini kwa ajili ya kuwekeza na kutalii.


“Rais Samia ‘anaupiga mwingi’, ameonyesha kwa vitendo kuwa wanawake wanaweza, nawaomba watanzania wenzangu tuendelee kumuunga mkono ili aweze kutimiza malengo aliyoyaweka kwa taifa hili, kwetu tunasema Samia mitano tena” amesisitiza Mama Kevela.


Akitolea mfano ujenzi wa shule, hospitali, zahanati miundombinu ya barabara za mijini na vijijini, ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR), Bwawa la kufua umeme la Nyerere, pamoja na madaraja yakiwemo ya Tanzanite Dar es Salaam pamoja na Daraja la Magufuli katika wilaya ya Misungwi ni kielelezo tosha cha juhudi zake za kuiletea maendeleo Tanzania.


Mwenyekiti huyo wa UWT Mkoa wa Njombe alisema miradi hiyo na mingine mingi inayoendelea nchini chini ya uongozi wa Rais Samia yanapaswa kupongezwa huku  akiwaomba watanzania  kumuombea kwa Mungu ili azidi kuampa afya njema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم